Uturuki katika Jumuiya ya Ulaya
13 Desemba 2004Wakati mawaziri hao wanakutana; maoni ya wananchi wa Ufaransa yanaonyesha kwamba asilimia 67 yao wanapinga Uturuki kujiunga na umoja huo wakati nchini Ujerumani asilimia 55 ya wananchi pia wanapinga. Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kuwa asilimia 54 ya raia wa UNfaransa wanakubali au wanaafiki kuanzishwa kwa mazungumzo hayo yenye lengo la Uturuki kujiunga na umoja huo. Wakati huo huo, uchunguzi uliofanywa na taasisi moja ya kuchukua maoni ya wananchi ya IFPO umeonyesha kuwa Uhispania inaunga mkono Uturuki kwa asilimia 65, uku italy nayo ikiunga pendekezo hilo la Uturuki kwa asilimia 49, ilhali asilimia 41 ya Uingereza ikiunga mkono pendekezo hilo, na wakati huo huo kupingwa na asilimia nyingine 30.Uchunguzi huo umeonyesha bayana jinsi rais wa Ufaransa, Jacque Chirac, anavyokabiliwa na upinzani mkali hasa kutoka upande wa wanachi kutokana na kuiunga mkono Uturuki kujiunga na Umoja huo. Rais huyo wa Ufaransa anajaribu kukwepa upinzani huo kwa kuchelewesha mazungumzo hayo hadi pale kura ya maoni itakapofanyika mwakani kuhusu katiba ya Umoja huo. Lakini wakati huo huo, alisema mkutano huo hautabainisha moja kwa moja Uturuki kuwa mwanachama.Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Joschka Fischer, alisema nikimnukulu: "mkutano huo hautapitisha uamuzi kuhusu Uturuki kujiunga na umoja huo. Uamuzi utakuja katika kipindi cha miaka kumi au hata miaka kumi na tano. Suala nyeti kwa sasa ni kuelekea kuijenga Uturuki",mwisho wa kunukulu. Lakini waziri wa mambo ya nje wa Uholanzi; Bernard Bot, ambaye nchi yake ndio rais wa umoja huo amesema kiini hasa cha mazungumzo hayo ni kuingizwa Uturuki ndani ya umoja huo. Hata hivyo, kikubwa kilichoonekana kuzua ubishi wa Uturuki kuwa mwanachama wa Umoja huo, kulingana na tasisi moja iliyofanya uchunguzi, ni Uturuki kutoheshimu haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kukiuka haki za wanawake pamoja na tofauti nyingi za kiutamaduni na dini. Suali la wasi wasi kwamba huenda Waturuki wengi watahamia katika mataifa hayo ya umoja wa ulaya halikupewa uzito sana lakini watu wanaotetea Uturuki kujiunga na umoja wa ulaya wanasema nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kisasa na kwamba inastahili kupewa nafasi ya kujiunga. Pamoja na hayo wanasema Uturuki ni sehemu ya bara la ulaya na itaimarisha sauti ya bara hili katika masuala ya kimataifa.
Saumu Mwasimba