Uturuki iko tayari kusimamia mazungumzo ya amani ya Ukraine
11 Mei 2025Uturuki imesema iko tayari kusimamia mazungumzo ya amani kati ya Ukraine na Urusi.
Soma pia:Trump kushirikiana na Erdogan kumaliza vita vya UkraineTangazo la Uturuki limetolewa Jumapili baada ya rais Vladmir Putin wa Urusi kubainisha kwamba nchi yake iko tayari kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Kiev na kupendekeza mazungumzo hayo yafanyike Istanbul.
Msimamo huo wa Urusi umekuja baada ya Ukraine kupendekeza siku 30 za kusitishwa vita kikamilifu kuanzia siku ya Jumatatu.
Rais Volodymyr Zelensky siku ya Jumapili(Leo) aliridhia pendekezo lililotolewa na Urusi la mazungumzo ya moja kwa moja lakini akisisitiza kwamba lazima kwanza vita visitishwe kikamilifu kwa muda kabla ya mazungumzo hayo.
Mwito wa Zelensky
Zelensky ameandika kwenye ukurasa wake wa X kwamba pendekezo la rais Putin la kuwa tayari kwa mazungumzo ya moja kwa moja ni ishara nzuri ambayo ulimwengu umekuwa ukiisubiri kwa hamu kwa muda mrefu.
Lakini akaongeza kwa kusema kwamba, hata hivyo hatua ya kwanza ya kumaliza vita kikamilifu ni kusitisha kwanza mapigano.
Wakati matumaini hayo yakiripotiwa, upande mwingine ripoti zimeeleza kwamba Urusi imeanzisha upya mashambulio makubwa ya droni nchini Ukraine Jumapili baada ya siku tatu za kutangaza kusitisha vita,kumalizika.
Imefanya mashambulizi 108 ya droni kutokea maeneo sita tofauti kwa mujibu wa jeshi la wanaanga la Ukraine ambalo limedhibitisha kudunguwa droni 60 huku nyingine 41 zikitajwa kushindwa kufikia shabaha yake.Soma pia: Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Poland ziarani nchini Ukraine
Wizara ya ulinzi ya Urusi hata hivyo imeishutumu Ukraine, kwamba ilikiuka makubaliano hayo ya Urusi ya usitishaji vita kwa siku tatu, zaidi ya mara 14,000.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa pamoja na Putin na kuwaambia kwamba nchi yake iko tayari kusimamia mazungumzo ya amani baina ya Urusi na Ukraine.
Soma pia:Ukraine yaripoti mashambulizi machache licha ya agizo la Putin la kusitisha mapigano kwa siku 3Putin ametowa pendekezo la kukubali mazungumzo ya moja kwa moja na Ukraine baada ya viongozi wa mataifa manne makubwa ya Umoja wa Ulaya,Ujerumani, Ufaransa,Uingereza na Poland kutishia kuzidisha shinikizo dhidi ya Moscow ikiwa haitokubali kusitisha vita kwa siku 30 bila masharti.
Emmanuel Macron, Keir Starmer,Friedrich Merz na Donald Tusk walikutana na Zelensky mjini Kiev katika ziara yao Jumamosi ya kuonesha mshikamano na Ukraine.