Utekaji wa wanaharakati Tanzania waitia wasiwasi Marekani
24 Mei 2025Ofisi ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani inayohusika na masuala ya Afrika imetoa wito wa uchunguzi wa haraka na wa kina kuhusu tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu. Na kuzihimiza nchi zote za Afrika Mashariki kuwawajibisha wale wanaohusika na ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mateso.
Wanaharakati mashuhuri Boniface Mwangi kutoka Kenya na Agather Atuhaire kutoka Uganda walisafiri kwenda Tanzania wiki hii kuonyesha mshikamano na kiongozi wa upinzani aliyekamatwa, Tundu Lissu, kabla ya kusikilizwa kwa kesi yake ya uhaini.
Hata hivyo, wao wenyewe walikamatwa kabla ya kufukuzwa nchini na baadaye kupatikana wakiwa wametelekezwa karibu na mpaka wa Tanzania. Mwangi na makundi ya kutetea haki za binadamu wanadai kuwa wote wawili waliteswa walipokuwa wakishikiliwa kwa siri bila mawasiliano kwa siku kadhaa.