Marekani yazitaka nchi 36 kuchukua hatua kwa raia wake
18 Juni 2025Taarifa ya kidiplomasia iliyotumwa na Wizara ya Mambo ya Nje mwishoni mwa wiki iliyopita, inazitaka balozi na balozi ndogo katika nchi 36 nyingi zikiwa za Afrika, kuchunguza nia ya nchi zao katika kuimarisha nyaraka za kusafiria za raia wao na kuchukua hatua za kushughulikia hali ya raia wao ambao wako Marekani kinyume cha sheria, ifikapo Jumatano.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Tammy Bruce amethibitisha kuwa mataifa hayo yanatakiwa kuimarisha mchakato wa kuchunguza pasi za kusafiria za raia wake, kuwakubali raia wao wanaorudishwa kutoka Marekani, na kuchukua hatua nyingine kuhakikisha raia wao sio kitisho kwa Marekani.
Nchi hizo 36 zilizoko kwenye tangazo hilo ni pamoja na Angola, Antigua na Barbuda, Benin, Bhutan, Burkina Faso, Cambodia, Cameroon, Cape Verde, Jamhuri ya Kidemokarsi ya Kongo, Djibouti, Dominica, Ethiopia, Misri, Gabon, Gambia na Ghana
Nchi nyingine ni Malawi, Mauritania, Niger, Nigeria, St. Kitts na Nevis, St. Lucia, Sao Tome na Principe, Senegal, Sudan Kusini, Syria, Tanzania, Tonga, Tuvalu, Uganda, Vanuatu, Zambia, Zimbabwe, Ivory Coast, Kyrgyzstan na Liberia.