Utafiti: Wanawake hawashiriki pakubwa kwenye siasa Afrika
20 Februari 2025Hayo yamebainishwa katika warsha ya wanahabari na wadau wa siasa chini ya wakfu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wanawake.
Ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi bado ni hafifu katika nchi za Afrika kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo unyanyasaji wa mitandaoni na mfumo dume unaozuia ushiriki wao.
Hayo yameelezwa katika warsha ya wanahabari kutoka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wanaokutana jijini Nairobi kujadili mapengo katika ushiriki wa kisiasa wa kundi hilo.
Akizungumza katika warsha hiyo, Josephine Mwangi, Meneja Programu wa mradi wa Ushiriki wa Wanawake katika Siasa, Afrika na Asia Magharibi kutoka taasisi ya IDEA, amesema ufinyu katika ushiriki wa kundi hilo katika siasa unachagizwa na sababu nyingi ikiwamo namna vyombo vya habari vinavyowamulika wanawake.
Soma pia:Harakati za kujenga uongozi wa wanawake Somalia
Ripoti ya African Barometer iliyochapishwa Novemba 2024 imeeleza kuwa, mwaka 2024 Afrika ilikuwa na asilimia 27 tu ya uwakilishi wa wanawake katika mabunge yote ya Afrika.
Kadhalika ripoti hiyo imeonyesha kuwa ongezeko la wanawake katika siasa Afrika limedumaa baada ya kuwepo kwa ongezeko la asilimia 1 tu, tangu 2021 hadi 2024.
Imeelezwa katika warsha hiyo, kuwa chanzo cha uwakilishi hafifu katika siasa kwa wanawake ni vitisho na unyanyasaji wanaposhiriki katika siasa, lakini hata wanapotumia mitandao ya kijamii.
Matumizi ya mitandao ya kijamii kwa wanawake
Katika ripoti hiyo, imeelezwa kuwa wanawake wengi wana wasiwasi wa kutumia mitandao ya kijamii wakihofia unyanyasaji na udhalilishaji.
Mshiriki katika warsha hiyo, mwanahabari Najjat Omar, amesema udhalilishaji mitandaoni ni moja ya chanzo cha ushiriki finyu wa kundi la wanawake kwenye majukwaa hayo.
Kadhalika washiriki wameelezwa kuwa kuna mapengo makubwa katika ushiriki wa siasa kwa wanawake wa vijijini kwa sababu wanakosa simu za kisasa za mkononi na mawasiliano ya intaneti yanayowawezesha kutoa mawazo yao kupitia mitandao ya kijamii.
Soma pia:Djinnit ahimiza wanawake wapewe nafasi za uongozi Afrika
Awali, mshauri mkuu na Demokrasia na Ujumuishi wa IDEA, Rumbidzai Kandawasvika-Nhundu alisema wanahabari hawana budi kutumia kalamu zao vyema ili kuhakikisha kuna ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.
Nhundu amesema licha ya katiba hizi kufanyiwa marekebisho, lakini yaliyoandikwa hayatekelezeki hivyo ni wajibu wa wanahabari kuripoti na kuibua masuala ya wanawake na uongozi.
Mengine yaliyoibuliwa katika Ripoti ya Afrika Barometer yanaonyesha kuwa wanaume wameendelea kushika nyadhifa za juu za kisiasa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita barani Afrika, huku wanawake 22 tu ndio wanaoshika nafasi za juu katika nchi 17 za Afrika, ambayo ni sawa na asilimia 32 tangu mwaka 1970. Florence Majani, DW-Nairobi.