Utafiti: Itikadi kali bado tishio katika jeshi la Ujerumani
20 Mei 2025Chini ya asilimia 1 ya wanajeshi wa Ujerumani wanashikilia mitazamo ya "msimamo mkali wa kulia wa kudumu," kwa mujibu wa utafiti mpya uliofanywa na Kituo cha Historia ya Kijeshi na Sayansi ya Jamii cha Bundeswehr (ZMSBw).
Utafiti huo umebaini kuwa ni asilimia 0.4 tu ya wanajeshi wanaoonyesha mitazamo ya msimamo mkali wa kulia. Kwa upande wa wafanyakazi wa kiraia wa jeshi, asilimia hiyo ni 0.8% — kiwango kidogo sana ukilinganisha na asilimia 5.4 ya watu walio na mitazamo kama hiyo katika jamii ya Ujerumani kwa ujumla, kwa mujibu wa waandishi wa ripoti hiyo.
Hata hivyo, ripoti hiyo imeonyesha kuwepo kwa mitazamo mingine yenye matatizo miongoni mwa wanajeshi: asilimia 6.4 wana mitazamo ya ubaguzi wa kijinsia wa wazi, na asilimia 3.5 wana mitazamo ya chuki dhidi ya wageni.
Kwa ujumla, utafiti huo unaonekana kuwa wa matumaini, hasa ikizingatiwa kuwa Bundeswehr imekuwa ikikumbwa na kashfa mbalimbali miaka ya hivi karibuni kuhusu mitandao ya siasa kali za mrengo wa kulia na njama za kigaidi zinazohusisha baadhi ya wanajeshi wake.
Soma pia: Jeshi la Ujerumani kufanyiwa mageuzi baada ya kashfa-Waziri
Mwaka 2022, Luteni wa jeshi la Bundeswehr aitwaye Franco A. alihukumiwa kwa kupanga kutekeleza kitendo kilichotajwa kuwa "kinatishia usalama wa taifa,” akiwa amejifanya mkimbizi kutoka Syria. Mwaka 2017, mtandao wa kikosi cha kushughulikia majanga na walioshukiwa kupanga mapinduzi ya kijeshi uligunduliwa, na baadhi yao walikuwa wanajeshi waliopo kazini na waliostaafu. Vyombo kadhaa vya habari nchini Ujerumani vimeripoti kuhusu uwepo wa "jeshi kivuli" ndani ya Bundeswehr ambalo limepuuzwa na Idara ya Ujasusi ya Jeshi (MAD).
Je, tafiti za hiari zinaweza kuaminika?
"Ndio, nadhani utafiti huu unatoa angalau ahueni fulani,” alisema Markus Steinbrecher, mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo, alipoulizwa na DW. "Lakini ukichukulia ile asilimia 0.4% kama uwakilishi, basi bado tuna mamia ya watu ndani ya jeshi walio na mitazamo ya itikadi kali.”
Hili linaendana kwa kiasi kikubwa na takwimu za MAD: kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi, mwaka 2023 kulikuwa na uchunguzi wa kesi 1,049 za kushukiwa kwa misimamo mikali ndani ya jeshi, ambapo 776 walihusishwa na siasa kali za mrengo wa kulia, 22 wa mrengo wa kushoto, na 51 walihusishwa na itikadi za Kiislamu zenye msimamo mkali. Bundeswehr kwa sasa inaajiri zaidi ya watu 260,000, wakiwemo wanajeshi 180,000 na wafanyakazi wa kiraia 80,000.
Soma pia: Bunge la Ujerumani laidhinisha bajeti kubwa kwa jeshi
Kwa ajili ya utafiti mpya wa ZMSBw, mahojiano zaidi ya 4,300 yalifanyika mwishoni mwa mwaka 2022 na wanajeshi wa ngazi mbalimbali, pamoja na mijadala midogo 18 ya vikundi katika vituo vya kijeshi vinane kote nchini Ujerumani.
Steinbrecher alikiri kuwa tafiti zinazotegemea ushiriki wa hiari zina mapungufu. "Watu wanaweza kuweka alama kokote wanapotaka, hata kama maoni yao halisi ni tofauti — tunalielewa hilo,” alisema. "Ndiyo maana katika hatua mbalimbali tuliweka mbinu za ziada kujaribu kubaini kiwango ambacho majibu ya kweli huenda yamefichwa.”
Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanatia shaka umuhimu wa utafiti huo. Anke Hoffstadt, mtafiti wa siasa kali za mrengo wa kulia kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya Maadili ya Maendeleo mjini Dusseldorf, alisema kuwa utafiti huo una misingi dhabiti ya kitaaluma, lakini akaeleza kuwa ZMSBw ni sehemu ya jeshi la Bundeswehr lenyewe.
"Wao ni huru na wanafuata viwango vya kisayansi, lakini bila shaka wamo ndani ya muundo wanaouchunguza,” Hoffstadt aliambia DW.
Hoffstadt pia alisema kuwa washiriki wa utafiti huenda waliathiriwa na muda wa ukusanyaji wa data — mwaka 2022 — wakati ambapo kulikuwa na uangalizi mkali wa kisiasa kuhusu siasa kali za mrengo wa kulia ndani ya Bundeswehr na polisi.
Mwaka 2020, Waziri wa Ulinzi wa wakati huo, Annegret Kramp-Karrenbauer, alivunja kikosi kizima cha KSK (kikosi cha vikosi maalum) mjini Calw baada ya kufichuliwa kwa tukio la "sherehe ya kichwa cha nguruwe.” Katika hafla hiyo ya mwaka 2017, wanajeshi walidaiwa kutoa saluti za Hitler, kuajiri makahaba, kusikiliza muziki wa mrengo mkali wa kulia, na kurushiana vichwa vya nguruwe.
Pia mwaka huohuo wa 2020, jeshi la Bundeswehr lilikiri kupotea kwa takribani risasi 60,000 ambazo hazikuweza kufuatiliwa.
"Kwa wakati huo, kila mtu ndani ya Bundeswehr alijua yuko chini ya darubini,” alisema Hoffstadt. "Utafiti huu si wa ovyo, wala haujaendeshwa kwa nia mbaya, lakini napendekeza usomwe kwa mtazamo wa ukosoaji.”
‘Wananchi waliovaa sare'
Waandishi wa utafiti huo pia walieleza kuwa watu wenye mitazamo ya mrengo mkali wa kulia "huonyesha nia kubwa ya kujiunga na jeshi” — ingawa hilo halimaanishi kuwa watafanikiwa kuingia jeshini. "Kuvutiwa hakumaanishi kuwa wataomba, na kuomba hakumaanishi kuwa watakubaliwa,” kama alivyosema Steinbrecher.
Kwa hakika, kuna vizingiti vikali: Waombaji wapya hulazimika kupitia uchunguzi wa kiusalama kabla ya kuwa makurutu. Aidha, sheria za faragha kwa madaktari wanaofanya uchunguzi wa afya husitishwa ili kuruhusu wao kuripoti michoro ya miilini (tattoos) inayoweza kuashiria mitazamo mikali.
Soma pia: Baerbock ahitimisha ziara yake Irak kwa kutembelea Bundeswehr
Wanajeshi wa Ujerumani hawawajibiki tu kulinda taifa na katiba yake — maarufu kama "Sheria ya Msingi" — bali pia wana wajibu wa kisheria wa kutetea kwa dhati haki za kidemokrasia. Hii inamaanisha, kwa mfano, kupinga waziwazi maoni ya chuki au misimamo ya itikadi kali. Kwa maneno mengine, wanajeshi wa Ujerumani wanapaswa kuwa "wananchi waliovaa sare,” walio na wajibu kamili wa kulinda katiba. Kushikilia baadhi ya mitazamo, kama vile kukana mauaji ya Holocaust, ni marufuku kabisa jeshini.
Licha ya hatua zilizowekwa, hofu bado ipo
Pamoja na kuwepo kwa hatua mbalimbali za kuzuia misimamo mikali jeshini, Anke Hoffstadt haamini kwamba Bundeswehr inafanya vya kutosha kuzuia mitazamo ya itikadi kali kuingia jeshini — hasa kwa kuzingatia hali ya sasa ambapo mitazamo ya mrengo mkali wa kulia imeanza kuzoeleka katika jamii pana, kama inavyoonekana kwenye umaarufu wa chama cha Alternative for Germany (AfD).
"Kumekuwa na ‘matukio ya mtu mmoja mmoja' mengi mno jeshini kiasi cha kwamba si rahisi kuamini kuwa hatua zilizopo zinatosha,” alisema. "Kuna semina nyingi, mikutano na mafunzo ya siasa, lakini katika kambi za kijeshi hakuna ufahamu wa kina kuhusu ugumu na ujanja wa mitazamo ya kisasa ya mrengo wa kulia.”
Kwa upande mwingine, Markus Steinbrecher haoni hali hiyo kwa mtazamo wa huzuni. Anasisitiza kuwa jeshi la Ujerumani lina hatua kali zaidi za kupambana na itikadi kali ikilinganishwa na mataifa mengi mengine.
Soma pia: Waziri wa ulinzi wa Ujerumani awapa moyo wanajeshi Mali
"Ninaamini hili sasa limekuwa kipaumbele,” alisema. "Ninashiriki katika mradi wa utafiti wa kimataifa na nchi wanachama wa NATO, na kwa mtazamo wa kitaalamu, Ujerumani inaongoza katika suala la kuzuia misimamo mikali.”
Hata hivyo, Steinbrecher alionya kuwa kwa kuwa serikali ya Ujerumani sasa inalenga kuongeza ajira jeshini — na pengine hata kurejesha aina fulani ya huduma ya lazima ya kijeshi — huenda ukaguzi wa kina ukawa mgumu zaidi kuutekeleza kwa viwango vya sasa.
"Hatuwezi kukaa mikono mapajani,” alionya Hoffstadt. "Tunaweza kusema, ‘ah, chini ya asilimia moja, basi tuko salama.' Lakini hilo linaweza kuwa tu kilele cha barafu. Lazima tuendelee kuuliza kuhusu barafu lote.”