Ususiaji kura wa upinzani wampa ushindi mkubwa Maduro
27 Mei 2025Matokeo ambayo bado hayajathibitishwa na Tume ya Uchaguzi ya taifa hilo la Amerika ya Kusini, CNE, yanaonesha kuwa vuguvugu la Chavismo lilioasisiwa na mtangulizi wa Rais Nicolas Maduro, marehemu Hugo Chavez, limechukuwa viti 23 kati ya 24 vya ugavana, huku likitwaa viti 256 kati ya 285 vya ubunge.
Miongoni mwa waliotangazwa washindi wa ubunge ni mke wa Rais Maduro, Cilia Flores, na mtoto wao wa kiume, Nicolas Maduro Guerra.
Soma zaidi: Chama cha Maduro kushinda ubunge, ugavana Venezuela
Muungano mkuu wa upinzani ukiongozwa na Maria Corina Machado uligomea uchaguzi huo, lakini kundi dogo la upinzani likiongozwa na mwanasiasa aliyewahi kuwania urais mara mbili, Henrique Capriles, liliamua kushiriki likihoji kuwa ugomeaji wa awali ulimsaidia Maduro kujichimbia madarakani badala ya kumuangusha.
Mwenyewe Capriles ameshinda kiti chake bungeni.