Ushuru wa Marekani wawatisha wazalishaji mvinyo Ujerumani
1 Aprili 2025Wazalishaji wa bidhaa hiyo kutoka taifa hilo la Ulaya wana wasiwasi kutokana na kuwa sehemu kubwa ya soko lao linapatikana Marekani, ambako mvinyo wa Ujerumani una sifa ya kipekee na wateja wake wa kudumu.
Hata hivyo wataalamu wa masuala ya uchumi wanaona kuwa vita vya kibiashara vinavyoendelea kati ya Ulaya na Marekani bado vinaweza kuepukika.
Constantin Richter anaelekea kwenye shamba lake la mizabibu katika Bonde la Moselle, ambalo limekuwa likirithiwa ndani ya familia yake kwa vizazi kumi sasa.
Katika shamba hilo analima mizabibu na familia yake iumekuwa ikiuza mvinyo nchini Marekani tangu mwaka 1830. Lakini sasa, Richter ana wasiwasi mkubwa kuhusu tishio la Rais Trump la kuweka ushuru wa hadi asilimia 200 kwa mvinyo unaoingizwa kutoka Umoja wa Ulaya.
"Tunasafirisha zaidi ya asilimia 30 ya mvinyo wetu kila mwaka nchini Marekani... na ikiwa kutakuwa na ushuru wa asilimia 200 biashara itaporomoka. Ushuru wa asilimia 200 kwa kila kitu... hakuna atakayenunua tena." anasema Richter.
Nyongeza ya ushuru yaleta mashaka juu ya hatma ya wazalishaji mvinyo
Mzozo huu unawakumba wazalishaji wa mvinyo Ujerumani wakiwa wanakabiliwa na kipindi kigumu, wakikabiliwa na gharama kubwa za uzalishaji, urasimu na ongezeko la uzalishaji wa mvinyo duniani, jambo linaloshusha bei.
Mvinyo wa Ujerumani umedumu sokoni kwa miaka sasa kutokana na ubora wake wa hali ya juu na sifa yake nzuri, lakini kwa sasa ni vigumu kudumisha faida na mauzo.
Tishio la ushuru wa Trump limeharibu hali ya biashara katika maonyesho makubwa ya biashara ya mvinyo nchini Ujerumani Düsseldorf, ambapo wengi wana hofu ya kuporomoka kwa mapato.
"Ushuru huu utakuwa ni janga kwa wauzaji kwa mauzo yetu nje ya nchi... hasa kwa Marekani ni soko letu kubwa kwa nje. Tunapata theluthi moja ya faida zetu kutoka Marekani. Hivyo hili litatuathiri pakubwa." anasema Ernst Büscher wa Taasisi ya Mvinyo Ujerumani.
Mnamo mwaka 2019 Rais Trump aliwahi kutoza mvinyo wa Ujerumani ushuru wa asilimia 25, na katika wakati huo wauzaji wa Ujerumani na waagizaji wa Marekani waligawana mzigo wa gharama hizo ili kufanikisha kuvuka kipindi hicho cha mpito. Kwa hivyo ushuru wa asilimia 200 wa sasa ni mzigo mwingine na huenda ukawa ni mgumu zaidi kuhimili.
Matumaini bado yapo kwa baadhi nchini Ujerumani, lakini yanatoka wapi?
Lakini kwa wengine, bado kuna matumaini… wanajaribu kuwa na mtazamo chanya.
"Vita kamili vya kibiashara kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya bado vinaweza kuzuilika. EU imetangaza ushuru wa kulipiza kisasi unaoanza Aprili Mosi… lakini hadi wakati huo, bado kuna nafasi ya mazungumzo. Pande zote mbili zinapaswa kutambua kuwa vita vya kibiashara vitawaumiza wote, na makubaliano yanapaswa kufikiwa.” anasema Dr. Samina Sultan ambaye ni Mtaalamu wa Uchumi nchini Ujerumani
Katika shamba lake la mizabibu huko Moselle, Constantin Richter pia anatumai kutapatikana suluhu… na anatarajia msaada mkubwa zaidi kutoka kwa serikali ya Ujerumani.
"Trump alipotoa tangazo la ushuru wa asilimia 200… mara moja, wanasiasa wa ngazi za juu, mawaziri wa biashara na mambo ya nje walitoa matamko kwa nchini Ufaransa na Italia… lakini hapa Ujerumani, hatujasikia chochote kutoka kwa serikali.”
Wazalishaji wa mvinyo nchini Ujerumani wamekumbwa na pandashuka chungu mzima hapo awali, kwa sasa wanayo matumaini kwamba wataweza kuvuka salama kwa hili pia.