Ushuru uliowekwa na Trump wawakasirisha viongozi Ulaya
11 Februari 2025Viongozi wa Ulaya wameghadhabishwa na hatua ya rais wa Marekani ya kutangaza kuweka ushuru kwa bidhaa za chuma na aluminia kutoka Ulaya.
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema uamuzi huo wa Marekani hautokaliwa kimya.
Kiongozi huyo wa juu wa Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema jumuiya hiyo ya wanachama 27 itachukuwa hatua kali kujibu hatua iliyochukuliwa na Marekani, akifafanuwa kwamba hatua za Umoja wa Ulaya zitakuwa za kulinda maslahi yake ya kiuchumi, wafanyakazi wake,biashara na wateja wake.
Katika ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wa X Von der Leyen amesikitishwa sana na Uamuzi wa Marekani ambao amesema haujazingatia haki kuelekea Umoja wa Ulaya na hautokaliwa kimya.
Kamishna wa masuala ya biashara katika Umoja huo wa Ulaya,Maros Sefcovic nae ameliambia bunge la Ulaya hii leo Jumanne kwamba Marekani itachochea mfumko wa bei kwa hatua yake hiyo ya kurudisha ushuru kwa bidhaa za Aluminia na Chuma.
Jumatatu rais Donald Trump alitangaza kuongeza ushuru kwa bidhaa za Aluminia na chuma kutoka asilimia 10 hadi asilimia 25 bila ya kuweka pembeni mataifa washirika, kama hatua ya juhudi zake za kufufua viwanda vya Marekani, hatua ambayo inatishia kuibuwa vita vya kibiashara duniani.
Kamishna wa masuala ya kibiashara wa Umoja wa Ulaya, Sefcovic anasema ushuru uliowekwa na Marekani hakuna utakayemfaidisha, lakini jumuiya hiyo bado inataka kutafuta namna ya kupata suluhisho la pamoja na Marekani, haraka iwezekanavyo, litakaloziletea ufanisi pande zote mbili.
Mataifa mengi ya Umoja wa Ulaya yana wasiwasi mkubwa kufuatia uamuzi wa Marekani , ikiwemo Ufaransa,Uhispania na Ujerumani ambazo zimeshaahidi kuchukuwa hatua za kulipa kisasi dhidi ya Marekani ambayo imesema hatua zilizochukuliwa zitaanza kutekelezwa March 4.
Rais Donald Trump akisaini amri ya rais ya kuongeza viwango vya ushuru kwa mataifa mbali mbali, katika ikulu ya WhiteHouse pia alisema atafikiria kuweka viwango vya ushuru kwa bidhaa za magari,vifaa vya kielektoniki na bidhaa za utengenezaji madawa.
Soma pia: Umoja wa Ulaya utakuwa tayari kwa mazungumzo magumu na MarekaniKansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema Umoja wa Ulaya utachukuwa uamuzi wa pamoja kama soko kubwa duniani,kuijibu hatua ya rais Donald Trump, ikiwa hakutokuwa na njia nyingine itakayochukuliwa na Marekani.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Noel Barrot amesema mataifa ya Ulaya hayapaswi kuchelea kutetea maslahi yao mbele ya vitisho vya Marekani, akiongeza kwamba kuanzisha vita vya kibiashara hakutampa faida mtu yoyote.
Mwenzake wa Uhispania Jose Manuel Albares naye amesema Umoja wa Ulaya utachukuwa hatua za kujibu na kutetea maslahi ya soko la pamoja la Umoja huo.
Katika muhula wake wa kwanza madarakani, Donald Trump aliwahi kutangaza ushuru wa asilimia 25 kwa chuma na asilimia 10 kwa aluminia zinazoingizwa Marekani.
Lakini baadae aliondowa sehemu ya vikwazo hivyo kwa mataifa mbali mbali washirika wa kibiashara wa Marekani,ikiwemo Canada,Mexico Umoja wa Ulaya na Uingereza.