Usalama waimairishwa Kampala kufuatia tishio la kigaidi
3 Juni 2025Hiyo ni ibada kwenye madhabahu ya Namugongo ambapo kila tarehe 3 mwezi Juni mahujaji kutoka ndani na nje ya Uganda hujumuika kuwaenzi wale wanaowataja kuwa mababu zao katika imani hiyo barani Afrika. Maelfu ya watu hutembea kwa miguu kutoka mataifa jirani wakifanya safari za siku kadhaa kufika mahala hapo kama sehemu ya ibada yao. Kile ambacho huzingatiwa zaidi ya serikali ya Uganda katika kipindi hiki ni usalama wa watu hao kwenye barabara kuu wanazopitia lakini pia sehemu za ibada.
Na kwenye siku ya maadhimisho, kile kinachodaiwa kuwa jaribio la shambulizi la kigaidi kimetokea ambapo mwanamume na mwanamke waliokuwa wakisafiria kwenye pikipiki wameuawa kutokana katika mripuko uliotikisa mitaa ya kiunga cha Munyonyo ambako kunapatikana madhabahu eneo hilo jirani na fukwe za ziwa Victoria. Kulingana na taarifa za vyombo vya usalama, watu hao walishambuliwa kwa kupigwa risasi walipokuwa wakikaribia kanisa hilo ambapo waumini walikuwa wanaanza ibada yao.
Imedaiwa kuwa walilenga kufanya mashambulio kwa mahujaji hao na wameuwa mita mia tatu tu kutoka kanisa hilo. Msemaji wa majeshi Kanali Chris Magezi amewambia wanahabari kwamba mshukiwa mwanamke aliyeuawa ana mahusiano na kundi la waasi la ADF linaloendesha harakati zake mashariki mwa Congo na ametaja majina ya babake anayedaiwa aliuawa katika jaribio lingine la shambulio la kigaidi mwaka 2021.
Ummah watolewa wito kubaki kuwa watulivu Uganda
Ama baada ya hapo, hali ya taharuki ilitanda sehemu mbalimbali za mji huku vyombo vya usalama vikiwatuma askari kuzidisha doria kwenye barabara na mitaa yote. Mkuu wa jeshi la polisi Abbas Byakagaba ametoa mwito kwa umma kubaki watulivu akitoa hakikisho kuwa wamedhibiti hali na hakuna tena shambulio litatokea.
"kumekuwepo na mripuko kwenye pikipiki lakini tunawahimiza watu wetu kubaki chonjo dhidi ya hali au kitu wanachokishuku katika mazingira yao na kuendelea na maadhimisho ya siku ya mashahidi kwani tunawahakikishia kwamba tumedhibiti hali," alisema Byakagaba.
Miaka 140 iliyopita mashahidi zaidi ya 45 wa Uganda waliouawa kikatili na kwa maagizo ya mfalme wa enzi hiyo wa Buganda Kabaka Mwanga. Kwa jumuiya ya waumini, hao ni kielelezo cha kiwango cha imani ya kikristo barani Afrika na kwenye mahubiri, viongozi wa kidini hutumia fursa hiyo kuwahimiza watu kuishi maisha adilifu. Mhubiri mkuu kwenye madhabahu ya kianglikani Mhashamu Stephen Kazimba Mugalu ameshtumu kukithiri kwa matumizi ya mihadharati na ulevi wa kupindukia miongoni mwa jamii.
"kukithiri kwa matumizi ya bangi, pombe, mihadharati na vinginevyo kunaangamiza maisha ya wengi, pamoja na kuvunja familia na kuzidisha uhalifu na matatizo ya afya ya akili," aliongeza kusema Kazimba Mugalu.
Rais Museveni ndiye amekuwa mgeni mkuu kwenye madhababu yote mawili ya Kiagilikani na kikatoliki. Lakini katika hotuba yake hakugusia kisa hicho cha mripuko.
DW Kampala