Urusi yautambua rasmi utawala wa Taliban, Afghanistan
8 Julai 2025Katika video iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, Waziri wa mambo ya nje wa Afghanistan Amir Khan Muttaqi alisema: “Uamuzi wa kishujaa wa kuitambua serikali ya Taliban ni mfano kwa wengine.
“Tumewapeleka wawakilishi wetu wa kidiplomasia wetu katika nchi ambamo tuna balozi, pili nchi hizo zilizowakubali mabalozi wetu imo Urusi, sasa wakati mchakao huo ukiendelea Urusi imekuwa ya kwanza kututambua, tunatumai hili litaendelea zaidi, tumeipokea vyema hatua hii na ni ishara nzuri ya kuendelea mbele, na itaboresha uhusiano wetu na Urusi,” alisema Muttaqi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imethibitisha taarifa hiyo kupitia ukurasa wake wa Telegram, kwa kusema kwamba kutambuliwa rasmi kwa Serikali ya Kiislamu ya Afghanistan kutaimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uchumi, mapambano dhidi ya ugaidi na biashara ya dawa za kulevya.
Wakati huohuo, China nayo imetoa kauli ya kuunga mkono hatua ya Urusi. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Mao Ning, alisema China inafurahia maendeleo mapya katika uhusiano kati ya Urusi na serikali ya mpito ya Afghanistan.
Ikiongeza kuwa Kama jirani wa jadi na rafiki wa Afghanistan, China inaamini kwamba Afghanistan haipaswi kutengwa na Jumuiya ya kimataifa.
Mao Ning aliongeza kuwa licha ya changamoto za ndani na za kimataifa, China haijawahi kukatisha uhusiano wa kidiplomasia na Afghanistan.
Wakosoaji wasema hatua ya Urusi ni ya kimkakati zaidi kuliko kujali haki za binaadamu
Kwa upande wake, Mariam Solaimankhil, aliyekuwa mbunge nchini Afghanistan na mkosoaji wa Taliban, alisema hatua hiyo ya Urusi inaonesha kuwa maslahi ya kimkakati bado yanapewa uzito zaidi kuliko haki za binadamu na sheria za kimataifa.
Afghanistan imepitia miongo kadhaa ya migogoro, ikiwemo uvamizi wa Kisovieti (1979–1989) na vita vya miongo miwili vilivyoongozwa na Marekani hadi ilipoondoa wanajeshi wake mwaka 2021, hatua iliyowarudisha Taliban madarakani.
Tangu wakati huo, Taliban wameweka sheria kali za Kiislamu na kukosolewa vikali kimataifa, hasa kutokana na kukandamiza haki za wanawake na wasichana.
Urusi tayari imeondoa jina la Taliban kwenye orodha ya makundi ya kigaidi na imempokea balozi alieteuliwa na kundi hilo. Rais Vladimir Putin aliwahi kuwaita Taliban “washirika katika mapambano dhidi ya ugaidi” mwaka 2024.
Wakati wa utawala wao wa awali kati ya mwaka 1996 hadi 2001, Taliban walitambuliwa rasmi na mataifa machache tu kama Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Pakistan. China na Pakistan wamepokea mabalozi wa Taliban lakini bila kutoa utambuzi rasmi wa serikali hiyo hadi sasa.