Peskov: Tutashiriki mazungumzo ya amani ya Ukraine, Istanbul
30 Mei 2025Dmitry Peskov amesema wajumbe hao watakuwa tayari siku ya Jumatatu kushiriki mazungumzo hayo ya duru ya pili yatakayofanyika nchini Uturuki. Ameongeza kuwa anatumai mapendekezo ya kuvimaliza vita yaliyotayarishwa na pande zote yatajadiliwa.
Siku ya jumatano Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov alitangaza mkutano huo wa siku ya Jumatatu, akisema ujumbe utakaoshiriki utakuwa ni ule ule uliohudhuria duru ya kwanza ya mazungumzo na ulioongozwa na mshauri wa rais na aliyekuwa waziri wa utamaduni wa Urusi Vladimir Medinsky.
Urusi yapendekeza mazungumzo mapya na Ukraine
Ukraine nayo kupitia ujumbe wake unaoongozwa na Rustem Umerov, imesema haipingi uwepo wa mazungumzo hayo lakini ingelitaka kwanza kuyaona mapendekezo ya Urusi kabla ya mkutano wenyewe kuanza jambo ambalo Urusi imelikataa kata kata.
Ukraine imesema tayari imetoa orodha ya mapendekezo yake wa Urusi, lakini Urusi imekataa kufanya hivyo ikisema mapendekezo hayo hayapaswi kujadiliwa hadharani kabla ya mkutano kuanza. Pande hizo mbili hasimu zilikutana mara ya mwisho katikati ya mwezi Mei mjini Istanbul ambao ulikuwa mkutano wao wa kwanza wa ana kwa ana tangu kuanza kwa vita hivyo miaka mitatu iliyopita. Mkutano huo ulipelekea kuachiwa kwa idadi kubwa ya wafungwa kutoka pande zote mbili.
Uturuki inatumai suluhu ya mgogoro wa Ukraine itapatikana karibuni
Mkutano huu wa siku ya Jumatatu unatarajiwa kutuwama tu katika usitishwaji wa mapigano.
Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Hakan Fidan, amesema anatumai Urusi na Ukraine zitafanikiwa kupata suluhu ya mgogoro uliopo wakati wa mazungumzo hayo.
"Tumefikia mahali pagumu na muhimu katika vita hivi. Kuna njia mbili mbele yetu. ama tupuuzie hali ilivyo na kuendelea na vita au tufikie makubaliano ya suluhu ya kudumu kabla ya mwaka kumalizika," alisema Hakan.
Ukraine na washirika wake wa Ulaya wameishutumu mara kwa mara Urusi kwa kujikokota katika juhudi za kutafuta amani huku ikiendelea kutanua majeshi yake Ukraine na kuendelea kudhibiti baadhi ya sehemu ya taifa hilo jirani. Washirika hao wa Ukraine ikiwemo Marekani wanendelea kutoa wito kwa Moscow kuridhia bila masharti pendekezo la kusitisha vita jambo ambalo Urusi bado ina mashaka nalo.
Reutes,afp,ap