Urusi yataka EU kuiondolea vikwazo ili kurejesha makubaliano
28 Machi 2025Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema Urusi inazitaka nchi za Magharibi kuondoa vikwazo kwa Benki yake ya Kilimo inayofahamika kama Rosselkhozbank, kama sharti la kurejesha makubaliano ya kuruhusu usafirishaji salama wa mizigo ya Ukraine kupitia Bahari Nyeusi. Peskov ameongeza kuwa, ikiwa nchi za Ulaya hazitaki kufuata njia hii, ina maana hazitaki kuelekea kwa pamoja kwenye njia ya amani itokanayo na juhudi za Marekani na Urusi.
Viongozi wa Ulaya walipokutana jana mjini Paris , walikataa kulegeza vikwazo ilivyowekewa Urusi kutokana na mashambulizi yake dhidi ya Ukraine. Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema ni wazi kwamba kwa sasa sio wakati wa kuondolewa kwa vikwazo bali vinapaswa kuzidishwa, huku Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akisema kuwa, kuondolewa kwa vikwazo itakuwa kosa kubwa na haitokuwa na maana yoyote bila ya kufikiwa kwa mpango wa amani.
Soma pia: Putin apendekeza utawala wa mpito Ukraine
Hayo yakiarifiwa, rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amefanya mazungumzo na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin na kujadili uwezekano wa kurejesha makubaliano hayo ya usafirishaji wa mizigo katika Bahari Nyeusi huku Erdogan akimueleza Putin kuwa ushirikiano kati ya Uturuki na Urusi ndio ufunguo wa kutatua mizozo iliyopo na kwamba kurejeshwa kwa makubaliano hayo kutasaidia pakubwa katika mchakato wa amani.
Urusi na Ukraine zatupiana lawama kwa mashambuzi
Urusi imeendelea kwa kulishutumu jeshi la Ukraine kwa kujaribu kushambulia kila siku miundombinu yake ya nishati ikisisitiza kuwa kwa sasa Urusi bado inaheshimu ahadi yake ya kutoilenga miundombinu ya nishati ya Ukraine licha ya madai ya Kyiv, ikiwa ni pamoja na leo Ijumaa kwamba Urusi imekiuka makubaliano hayo. Peskov hata hivyo amesema Urusi bado inayo haki ya kujiondoa kwenye makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Marekani ikiwa Ukraine haitoyaheshimu:
"Itakuwa haina maana kwetu kuheshimu makubaliano hayo wakati kila usiku tunashuhudia majaribio ya mashambulizi kwenye miundombinu yetu ya nishati. "
Soma pia: Waziri Wang Yi wa China kufanya ziara Urusi wiki ijayo
Mamlaka katika mikoa kadhaa ya kusini mwa Ukraine zimeripoti kwamba vifaa kadhaa vya mitambo ya nishati vimeharibiwa kufuatia msururu wa mashambulizi ya droni zipatazo 100, na kwamba mashambulizi hayo ni wazi lilikuwa jaribio la kudhoofisha uthabiti wa miundombinu ya nishati nchini Ukraine. Kwa upande wake Urusi imesema Ukraine imeharibu mtambo mkubwa wa gesi katika mji wa Sudzha.
(Vyanzo: Mashirika)