Urusi yaituhumu Ukraine kwa kukishambulia kinu cha nyuklia
25 Agosti 2025Maafisa wa Urusi walisema vituo kadhaa vya umeme na nishati vililengwa katika mashambulizi ya usiku kucha Jumamosi. Moto kwenye kinu cha nyuklia ulizimwa haraka bila majeruhi wowote kuripotiwa. Licha ya kuwa shambulizi hilo liliharibu transfoma, viwango vya mionzi vilibaki katika vipimo vya kawaida.
Shirika la Umoja wa Mataifa la matumizi ya nishati ya nyuklia lilisema linafahamu ripoti hizo vya vyombo vya habari lakini halikuwa limepokea uthibitisho rasmi na huru. Mkuu wa shirika hilo la IAEA Rafael Mariano Grossi alisema kila kituo cha nyuklia lazima kilindwe wakati wote. Ukraine haikuzungumzia maramoja habari za shambulizi hilo.
Siku nyingine ya Uhuru katikati ya vita
Matukio hayo yalijiri wakati Ukraine ikiadhimisha Siku ya Uhuru. Ukraine ilitangaza uhuru wake mwaka wa 1991 kutoka kwa Muungano wa Sovieti. Rais Volodymyr Zelensky alitoa hotuba ya video katika Uwanja wa Uhuru mjii Kyiv akisisitiza dhamira ya taifa hilo
"Na kila siku, tunarudisha zaidi na zaidi vita hivi mahali vilikotoka. Katika anga ya Urusi na kwenye ardhi ya Urusi. Na kwa kila hatua ya vita hivi huko, kukiwa na shinikizo kwa Urusi, pamoja na hasara halisi wanayopata, tunajua kwamba amani kwa Ukraine inakaribia."
Alisisitiza kuwa mkutano kati yake na Rais wa Urusi Vladimir Putin ndio njia bora zaidi ya kusonga mbele. Mjumbe maalum wa Marekani Keith Kellogg alihudhuria maadhimisho hayo, ambapo Zelensky alimtunuku Tuzo ya Juu kabisa ya heshima. Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney aliwasili Kyiv jana asubuhi kwa mikutano na Zelensky.
Kwenye mkuatano wa Pamoja wa waandishi Habari na Zelensky, Carney alisema Canada itawekeza dola bilioni 2 za Canada katika msaada mpya wa kijeshi kwa Ukraine ili kuimarisha jeshi lake na kutoa silaha zinazohitajika kwa dharura.
"Tunashauriana na washirika wetu na muungano wa walio tayari, na Ukraine, kuhusu taratibu za dhamana hizo za usalama, wa ardhini, angani na baharini. Na siwezi kufuta uwekezano wa uwepo wa askari nchini Ukraine."
Norway kupitia Waziri Mkuu Jonas Gahr Store ilitangaza jana msaada mpya muhimu wa kijeshi wa karibu dola milionin 695 kwa ajili ya mifumo ya ulinzi wa angani.
Mabadilishano ya wafungwa
Wakati huo huo, askari wa Urusi waliendelea kusonga ndani mashariki na kaskzini mwa Ukraine, ambako Urusi ilidai Jumamosi kuwa askari wake walivitwaa vijiji viwili katika mkoa wa Donetsk. Idara ya Intelijensia ya Wizara ya Ulinzi ya Ukraine imesema Jumapili kuwa Ukraine imevikomboa vijiji vitatu.
Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema kuwa askari 146 wa Urusi walirejeshwa kutoka Ukraine, kwa kubadilishana na idadi sawa na hiyo ya askari wa Ukraine.
AP