Urusi yasema sio rahisi kufikia amani ya Ukraine na Marekani
15 Aprili 2025Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye anasema anataka kukumbukwa kama mleta amani, amekuwa akisema mara kwa mara kuwa anataka kufikia kikomo cha umwagaji damu kwa vita vya miaka mitatu nchini Ukraine, ingawa mwafaka bado haujapatikana.
Sasa Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema sio rahisi kufikia vipengele muhimu vya makubaliano. Lavrov amesema hayo katika mahojiano na gazeti la Kommersant alipoulizwa kama Moscow na Washington zimekubaliana kuhusu masuala kadhaa ya mwafaka unaosakwa wa amani. Lakini amesema majadiliano bado yanaendelea.
Siku ya Jumanne, mjumbe maalum wa Trump alisema kuwa rais wa Urusi Vladmir Putin yuko tayari kwa makubaliano ya "amani ya kudumu" na Ukraine.
Steve Witkoff alikutana Ijumaa na Putin mjini Saint Petersburg– mkutano wao wa tatu tangu rais huyo Mrepublican aliporejea kwenye Ikulu ya White House mwezi Januari.
Witkoff amesema katika mahojiano yaliyorushwa jana na tevelisheni ya Marekani ya Fox News kuwa anahisi mpango wa amani unakaribia kupatikana. Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov alisema mazungumzo kati ya viongozi hao wawili ni muhimu sana."Mada ya mkutano (kati ya Putin na Trump) haijajadiliwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu mkutano wowote lazima uwe umeandaliwa vyema. Mada zinazojadiliwa ni ngumu sana, kwa hivyo itakuwa vigumu sana kudhani kutakuwa na matokeo yoyote ya haraka."
Soma pia: Viongozi wa dunia walaani shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Lavrov anasema msimamo wa Urusi uliwekwa wazi na Rais Putin mnamo Juni 2024 wakati Putin alipotaka Ukraine iyafute rasmi malengo yake ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO na kuwaondoa askari wake kutoka kwenye maeneo yote manne ya Ukraine yaliyokwapuliwa na Urusi.
Kwingineko, China leo imepinga kile ilichokiita ni "udanganyifu na upotishaji" kuhusiana na raia wake wawili waliokamatwa nchini Ukraine, baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kuishutumu Moscow kwa kuiingiza Beijing katika uvamizi wake. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Lin Jian amesema China inazichunguza habari na mazingira husika ili kubaini ukweli kuhusu wafungwa wa kivita wa China.
Kwenye uwanja wa mapambano, vikosi vya Kyiv vimeupiga mkoa wa Kursk wa Urusi unaopakana na Ukraine vikitumia mamia ya ndege zisizoruka na rubani. Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema ilizidungua droni 109 katika mkoa wa Kurski usiku wa kuamkia leo. Mtu mmoja aliuawa na wengine tisa kujeruhiwa. Majengo kadhaa Katikati mwa mji pia yaliharibiwa kwa moto.
AFP, DPA, Reuters