Urusi yasema itaendelea kuzungumza na Marekani
14 Julai 2025Mjumbe wa rais wa Urusi,Vladimir Putin kuhusu uwekezaji, Kirill Dmitriev amesema, mazungumzo kati ya Urusi na Marekani yataendelea licha ya kuweko juhudi za kujaribu kuyakwamisha.
Matamshi hayo yamechapishwa kwenye ukurasa wa Telegram wakati rais Donald Trump akitarajiwa leo Jumatatu kutangaza kile kimetajwa kuwa Taarifa kubwa.
Rais huyo wa Marekani hivi karibuni alionesha kufadhaishwa na rais Putin kuhusiana na suala la vita vya Ukraine.
Jana Seneta wa Republican Lindsey Graham alikiambia kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani, kwamba nchi hiyo huenda hivi karibuni ikabadili mwelekeo wa sera zake kuelekea Urusi.
Graham amesema kwa miezi rais Trump amekuwa akijaribu kumshawishi Putin na ameendelea kuuwacha wazi mlango wa mazungumzo na Urusi lakini mlango huo unakaribia kufungwa.
Hivi leo mjumbe maalum wa Trump kuhusu Ukraine Luteni jenerali mstaafu Keith Kellog amewasili Kiev.