Urusi yasema itaisaidia Iran
23 Juni 2025Jumuiya ya kimataifa bado inatafuta jibu la namna ya kuushughulikia mzozo kati ya Israel na Iran, japo mashambulio yanaendelea kwa pande zote mbili.
Israel imeshambulia majengo ya serikali ya Iran mjini Tehran hivi leo, baada ya Iran nayo kufanya msururu wa mashambulio ya makombora na droni dhidi ya Israel.
Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na viongozi mbali mbali wa ulimwengu wamezungumzia wasiwasi ulioko kuhusu hatma ya vita hivi.
Mashambulio ya kulipiziana kisasi kati ya Iran na Israel bado yanaendelea kwa kiwango cha kasi, jeshi la Israel likisema limeshambulia majengo kadhaa ya serikali katika mji mkuu wa Iran, Tehran, na kuthibitisha pia kuzishambulia barabara za kwenye eneo la kituo cha nyuklia chaFordo, kwa lengo la kuzuia shughuli zozote za kukifikia kinu hicho cha urutubishaji urani.
Iran imefyetuwa makombora chungu nzima na droni kuelekea miji ya Israel baada ya Marekani kuvishambulia vituo vyake vya nyuklia kikiwemo hicho cha Fordo mwishoni mwa wiki, ambacho kimejengwa chini kwa chini ya milima.
Wizara ya ulinzi ya Israel inasema imeshambulia mpaka gereza hatari la Evin pamoja na makao makuu ya jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran. Kufuatia hali inayoendelea hivi sasa, Ubalozi wa Marekani nchini Qatar umetowa tangazo la tahadhari ukiwataka raia wake nchini humo watafute mahala salama pa kujihifadhi mpaka litakapotolewa tangazo jingine.
Tahadhari ya Marekani
Ubalozi huo hata hivyo haukufafanuwa zaidi wala kujibu maswali ya waandishi habari, ingawa tangazo hilo limekuja huku hali ya wasiwasi ikiwa imeongezeka Mashariki ya Kati, baada ya Marekani kuishambulia Iran usiku wa kuamkia jana Jumapili,Iran ikiapa kuchukua hatua.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ameiunga mkono hatua ya Marekani na Israel akisema haoni sababu ya kukosowa mashambulio yaliyofanywa na mataifa hayo washirika wa Ujerumani.
"Tangu wiki iliyopita, kwa zaidi ya wiki sasa vita vya wazi vimekuwa vikiendelea katika Mashariki ya Kati. Nataka kuweka wazi kwenye hili. Hakuna sababu kwetu na kwangu binafsi kukosoa kile ambacho kimeanzishwa na Israel wiki moja iliyopita na wala hakuna sababu ya kukosoa kilichofanywa na Marekani mwishoni mwa juma. Ndio hatari haikosekani, lakini kuacha mambo kama yalivyokuwa pia halikuwa chaguo.''
Vita kati ya Iran na Israel na uingiliaji kati wa Marekani kwa kuishambulia Iran vimeongeza wasiwasi duniani na hasa baada ya bunge la Iran kuidhinisha hatua ya kuufunga Mlango Bahari wa Hormuz unaotegemewa na ulimwengu katika usafirishaji mafuta.
Wasiwasi wa Jumuiya ya Kimataifa
China, Umoja wa Ulaya na viongozi mbalimbali wamezungumzia juu ya umuhimu wa kufanyika juhudi za kuishawishi Iran kutochukuwa hatua hiyo.
Pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani amesema amezungumza na mwenzake wa Iran, Abbas Araghchi, na kumwambia hatari zinazoweza kusababishwa na hatua ya kuifunga njia hiyo ya Hormuz, ikiwemo kuuharibu uchumi wa Iran yenyewe na mataifa mengi yote ya ulimwengu, ikiwemo China.
Urusi, mmoja wa washirika wa karibu wa Iran, imesema inatazama namna inavyoweza kuisaidia Iran kujiondowa katika hali inayoendelea.
Araghchi alikutana na Rais Vladmir Putin hivi leo mjini Moscow na kumpa hakikisho hilo huku akiyaita mashambulio ya Israel na Marekani kuwa ya uchokozi usiokuwa na sababu.
Rais Donald Trump pamoja na kuishambulia Iran amezungumzia pia uwezekano wa kuchochea mabadiliko ya kiutawala kwenye Jamhuri hiyo ya Kiislamu, fikra ambazo imeshaanza kupewa nguvu katika nchi za Magharibi.
Kituo cha utangazaji cha Ufaransa, RFI, kimemuhoji mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel raia wa Iran, Shirin Ebadi, aliyekimbilia uhamishoni nchini Uingereza, ambaye amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribia kabisa kuporomoka, ingawa akasema mapinduzi ya utawala wa Iran yanaweza kufanywa na watu wenyewe wa Iran na sio nguvu kutoka nje.
Wakati huo huo, khofu inaongezeka kuhusu uharibifu na athari zinazoweza kutokea katika kituo cha nyuklia cha Fordo, baada ya mashambulio ya Marekani, huku mashirika mbalimbali ya ndege duniani yakitangaza kufuta au kupunguza safari zao za Mashariki ya Kati.