Urusi yasema haitojadiliana kuhusu mikoa mitano iliyoinyakua
27 Februari 2025Msemaji wa Ikulu ya Urusi ya Kremlin Dmitry Peskov amewaambia waandishi wa habari kuwa maeneo ambayo kwa sasa yapo chini ya himaya ya Shirikisho la Urusi na ambayo yameorodheshwa kwenye katiba ya nchi hiyo, ni maeneo yasiyoweza kutenganishwa na Urusi na kwamba hilo halipingiki na kamwe haliwezi kujadiliwa.
Maeneo hayo ni rasi ya Crimea iliyonyakuliwa mwaka 2014 kufuatia operesheni fupi ya kijeshi na kura ya maoni ambayo ilitajwa kutokuwa halali na serikali mjini Kyiv pamoja na mataifa ya Magharibi.
Baada ya kuanzisha uvamizi kamili nchini Ukraine mwezi Februari mwaka 2022, Urusi ilitangaza mwezi Septemba kuwa imetwaa mikoa minne ya Ukraine ya Donetsk, Lugansk, Zaporizhzhia na Kherson, licha ya kutokuwa na udhibiti kamili wa mikoa hiyo.
Juhudi zaendelea ili kuvimaliza vita hivyo
Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na rais wa baraza la umoja huo Antonio Costa watahudhuria mkutano wa Jumapili hii mjini London utakaojadili mzozo wa Ukraine na usalama wa Ulaya. Viongozi hao wakuu wa taasisi yenye nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya, wataungana pia na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na viongozi wengine wa Ulaya katika mazungumzo yaliyoandaliwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ambaye leo hii yuko ziarani nchini Marekani.
Soma pia: Marekani na Ulaya zaendeleza juhudi ya kuutatua mzozo wa Ukraine
Katika hatua nyingine, Moscow na Washington wameendelea na mazungumzo mjini Istanbul ili kurekebisha mahusiano yao ya kidiplomasia. Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema leo Alhamisi kuwa mazungumzo ya kwanza yaliyofanyika kati ya nchi yake na utawala mpya wa Marekani yanatoa matumaini ya kutatua matatizo kama vile mzozo wa Ukraine.
" Ningependa kueleza kwamba mawasiliano ya kwanza na utawala mpya wa Marekani yametoa matumaini kwa kiasi fulani. Kuna dhamira ya pande zote zinadhamiria kuurejesha uhusiano kati ya mataifa yetu mawili na kuutatua polepole mlima mkubwa wa matatizo ya kimkakati katika mfumo wa kimataifa."
Soma pia: Macron awaambia wenzake wa EU alichozungumza na Trump
Putin amesisitiza kuwa kunadhihirika nia ya pande zote ya kushughulikia suala la kurejesha mahusiano mema. Awali Kremlin ilisema kuwa mazungumzo na Marekani yanapaswa kuendelea lakini hakuna anayetarajia suluhu ya haraka.
Aidha, Waziri Mkuu wa Ireland Micheál Martin atakutana kwa muda katika uwanja wa ndege wa Shannon na Volodymyr Zelensky kabla ya rais huyo wa Ukraine kusafiri kuelekea nchini Marekani ambapo anapanga kukutana siku ya Ijumaa na Rais wa Marekani Donald Trump ili kukamilisha makubaliano yatakayoiruhusu Marekani kujipatia madini ya Ukraine. Ufaransa pia imetangaza kuwa inalenga kupata madini hayo muhimu ya Ukraine na kuwa mazungumzo yanaendelea kwa miezi kadhaa sasa.
(Vyanzo: DPA, AP, Reuters, AFP)