Urusi yapuuzilia mbali vikwazo vipya vya EU
18 Julai 2025Nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zilitangaza duru ya 18 ya vikwazo vinavyolenga kuiwekea shinikizo Ikulu ya Kremlin kwa kupunguza zaidi mapato ya Urusi yatokanayo na usafirishaji wa mafuta kwa nchi zisizo wanachama wa Umoja wa Ulaya na hivyo kuiathiri sekta ya kifedha ya Urusi. Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amevipuuzilia mbali. "Wakati huo huo, tumepata kinga fulani kutokana na vikwazo, tumezoea kuishi chini ya vikwazo. Tutahitaji kuchanganua duru mpya ya vikwazo ili kupunguza madhara yake. Zaidi ya hayo, kila kifurushi kipya cha vikwazo kinaongeza madhara kwa nchi zinazojiunga na mpango huo."
Duru mpya ya vikwazo inalenga kupunguza ukomo wa bei ya mafuta uliowekwa na kundi la G7 wa kununua mafuta ghafi yaUrusihadi dola 47.6 kwa pipa.
Hatua hizo mpya ziliidhinishwa baada ya Slovakia kutupilia mbali kizuizi chake cha wiki nzima kufuatia mazungumzo na Umoja wa Ulaya kuhusu mipango tofauti ya kuondokana na uagizaji wa kutoka Urusi. Akizungumza mjini Paris baada ya kukutana na waziri mwenzake wa Ujerumani Johan Wadephul, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Jean-Noel Barrot amepongeza kupitishwa kwa vikwazo hivyo. "Msaada huu (kwa Ukraine) unahusisha hasa kuendeleza kupeleka silaha za kuiwezesha Ukraine kujilinda, pamoja na kuweka vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Urusi ili kumaliza rasilimali zinazoiwezesha kufadhili vita vyake.
Umoja wa Ulaya pia uliyalenga mabomba ya gesi yanayopita chini ya Bahari ya Baltic ya Nord Stream kati ya Urusi na Ujerumani ili kumzuia rais Vladmir Putin kutengeneza mapato yoyote kutokana na mradi huo katika siku za usoni.
Wakati huo huo, Peskov amesema Moscow inakaribisha kauli za Zelensky kuhusiana na uwezekano wa kuwepo mazungumzo ya amani. Zelensky awali alisema kuwa mchakato wa mazungumzo unahitaji kupewa msukumo zaidi.
Urusi na Ukraine zilifanya duru mbili za mazungumzo ya amani nchini Uturuki mapema mwaka huu ambayo yaliwezesha makubaliano ya kubadilishana wafungwa wa kivita na miili ya askari waliouawa vitani. Lakini hakuna tarehe iliyotangazwa ya duru ya tatu ya mazungumzo na pande zinazozozana bado hazijakubaliana kuhusu masharti ya kusitishwa mapigano au kupatikana amani hatimaye.
AFP, Reuters