Urusi yapinga dhamana ya Usalama kwa Ukraine
29 Agosti 2025Mawaziri wa Ulinzi wa Umoja wa Ulaya wamewasili mjini Copenhagen nchini Denmark kuhudhuria mkutano usio rasmi ambako watajadili maswala yanayohusu kuimarisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine, utayari wa ulinzi wa Ulaya, misheni za Umoja wa Ulaya na pia hali ya Mashariki ya Kati.
Kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine washirika wa nchi hiyo kutoka nchi za Ulaya wanakusanya na kuiweka pamoja mikakati ya dhamana ya usalama kwa Ukraine hatua ambayo inaweza kuwa sehemu ya mchakato wa amani na kwa ajili ya kuilinda Ukraine dhidi ya uwezekano wa mashambulizi kutoka Urusi katika siku za baadae.
Hata hivyo Urusi imesema mapendekezo ya nchi za Magharibi kuhusu dhamana ya usalama wa Ukraine yanaegemea 'upande mmoja' na ni hatari iwapo mapendekezo hayo yatazingatiwa kwa sababu yataongeza migogoro kati ya Urusi na nchi za Magharibi kutokana na kwamba Ukraine itageuzwa kuwa eneo la "uchochezi wa kimkakati" kwenye mipaka ya Urusi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharov, amesema leo siku ya Ijumaa kwamba "Dhamana ya usalama lazima iwe na msingi wa kufikia makubaliano yanayozingatia pia usalama wa Urusi na maslahi yake."
"Masharti yasiyokubalika hayapaswi kupokelewa"
Amesema Moscow ilishasema hapo awali kwamba inayapinga mapendekezo hayo ya Ulaya na haitakubali uwepo wowote wa askari wa NATO kwenye eneo lolote nchini Ukraine.
Waziri wa Ulinzi wa Latvia Andris Spruds, amesema, masharti yasiyokubalika hayapaswi kupokelewa. Isipokuwa masharti ambayo yanakubaliwa na upande wa Ukraine ndiyo yanapaswa, kuungwa mkono na Umoja wa Ulaya.
Mkutano wa leo wa Mawaziri wa Ulinzi wa Umoja wa Ulaya utafuatiwa hapo kesho na Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje, utakaoongozwa na Denmark, ambayo ndio mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya.
Vyanzo: RTRE/AFP