Urusi yakosoa kauli ya Merz iliyomtaja Putin kuwa mhalifu
3 Septemba 2025Ikulu ya Urusi Kremlin imesema hivi leo kuwa mapendekezo yote ya Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz kuhusu mchakato wa amani katika mzozo wa Ukraine , yanapaswa kupuuzwa baada ya Moscow kusema imeshuhudia mfululizo wa matamshi "yasiofaa" ya Merz dhidi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ProSieben.Sat1, Merz alisema kuwa Putin huenda ndiye mhalifu mkubwa wa kivita wa nyakati hizi, na kwamba watu kama hao hawafai kupewa ahueni. Matashi yaliyokosolewa vikali na Moscow ambayo inakanusha kitendo cha kuvihusisha vikosi vyake na uhalifu au kwamba Putin aliwahi kutoa amri yoyote katika operesheni ya kijeshi nchini Ukraine ambayo inaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov akiwa ziarani nchini China amesema Urusi haiwezi kuzingatia pendekezo la hivi majuzi la Merz aliyesema kuwa mji wa Geneva unafaa kuwa mahali pa mazungumzo ya amani kati ya Ukraine na Urusi, hasa kutokana na kauli zake dhidi ya Putin.
Mapigano yaendelea kuripotiwa
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi iliishambulia nchi hiyo usiku wa kuamkia Jumatano kwa zaidi ya droni 500 na dazeni mbili za makombora, huku miundombinu ya kiraia hasa ile ya nishati ikilengwa zaidi katika maeneo ya magharibi na katikati mwa Ukraine.
Rais wa Ukraine na viongozi wa Ulaya wanaendelea na mazungumzo yenye dhamira ya kuimarisha ulinzi wa Ukraine na kuongeza kasi kwenye juhudi za amani zinazoongozwa na Marekani ambazo hadi sasa hazijafanikiwa kuzaa matunda. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas ameilaumu Urusi kwa kuuendeleza mzozo huo:
"Ni wazi kwamba Urusi haina nia ya dhati ya kuvimaliza vita hivi. Na tumeshuhudia tena mashambulizi ya usiku wa jana dhidi ya Ukraine. Kwa hivyo tunapaswa kushughulikia matokeo ya hali hii kwa Ulaya. Na njia mojawapo ni kutoa msaada zaidi wa kijeshi, kidiplomasia na kiuchumi kwa Ukraine na hasa wakati wa usitishwaji mapigano. Jeshi imara la Ukraine ndio hakikisho kubwa zaidi la usalama na ndiyo maana tunatoa mafunzo kwa wanajeshi pamoja na msaada wa kifedha na vifaa."
Siku ya Alhamisi (04.09.2025), viongozi wa Ulaya watakutana mjini Paris-Ufaransa katika kile kinachofahamika kama "muungano wa walio tayari" kuisaidia Ukraine. Ujerumani imesema katika mkutano huo, viongozi hao watawasiliana kwa njia ya simu na Rais wa Marekani Donald Trump. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Mark Rutte amesema anatarajia kuwa mkutano huo wa kesho huko Paris utaweka bayana suala la hakikisho la usalama kwa Ukraine.