Urusi yaishambulia Ukraine kwa makombora 30 na droni 300
19 Julai 2025Shambulio hilo limesababisha kifo cha mtu mmoja na kuharibu miundombinu muhimu ya kiraia huko Odessa na Sumy , na limepelekea pia kukatika kwa umeme katika maeneo hayo na kuwaathiri maelfu ya familia.
Wakati huohuo, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imefanikiwa kudungua droni 13 zilizorushwa na Ukraine na kuelekezwa katika mji mkuu Moscow. Hata hivyo Meya wa mji huo Sergei Sobyanin hakutoa taarifa yoyote kuhusu majeruhi au uharibifu uliotokea.
Urusi imesema pia kuwa imedungua zaidi ya droni 80 zilizorushwa na Ukraine usiku wa kuamkia Jumamosi hasa katika maeneo ya mpakani. Hata hivyo shughuli za usafiri zilitatizika katika viwanja vya ndege vya Moscow vya Domodedovo na Sheremetyevo.
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, Ukraine imekuwa ikikabiliana na uvamizi wa Urusi na imekuwa ikitoa miito kwa washirika wake wa Magharibi kuipatia silaha zaidi na kuiruhusu kushambulia hadi maeneo ya mbali ndani ya Urusi.