Urusi yaishambulia miji mitatu nchini Ukraine
22 Julai 2025Vikosi vya Urusi vimeishambulia usiku wa kuamkia leo miji mitatu nchini Ukraine na kusababisha kifo cha mtoto mmoja na kuwajeruhi watu wengine 24. Mashambulizi hayo yamefanyika siku moja tu kabla ya kufanyika kwa duru ya tatu ya mazungumzo ya moja kwa moja ya amani yaliyopangwa kati ya ujumbe kutoka Moscow na Kyiv.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameeleza jana Jumatatu usiku uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo kati ya ujumbe wa Kyiv na Moscow japo ameonyesha kutokuwa na matumaini kwamba yangeleta maendeleo yoyote katika kuvimaliza vita hivyo vilivyodumu miaka mitatu sasa.
Hii ni licha ya juhudi za utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump za kujaribu kuvimaliza vita hivyo, huku juhudi za kiongozi huyo wa Marekani zikishindikana hadi sasa kutokana na msimamo usiyoyumba wa Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Duru mbili za mazungumzo zilifanyika mjini Istanbul, huku vyombo vya habari vya Urusi vikiripoti kwamba mji mkuu huo wa Uturuki huenda ukatumika tena kuandaa duru ya tatu ya mazungumzo.
Mazungumzo ya amani yawekewa matumaini madogo
Zelenskiy amesema, "Leo nimejadili na Rustem Umerov juu ya maandalizi ya mpango wa kubadilisha wafungwa na mkutano mwengine na ujumbe wa Urusi nchini Uturuki. Umerov amesema mkutano huo umepangwa kufanyika Jumatano, maelezo zaidi yatatolewa kesho."
Mazungumzo ya awali yaliyofanyika mwezi Mei na Julai yalikuwa na mafanikio kidogo kwani yaliwezesha ubadilishanaji wa wafungwa wa vita na miili ya wanajeshi waliouawa, lakini hayakuwezesha makubaliano mengine.
Wakati mazungumzo hayo yanaposubiriwa, vita vinaendelea bila kukoma. Urusi inaendelea kuishambulia kwa nguvu Ukraine katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Moscow pia inafyetua makombora na kutumia droni kuishambulia miji kadhaa ya Ukraine hasa nyakati za usiku.
Kuanzia usiku wa kuamkia Jumatatu, Urusi ilifyetua makombora kuelekea maeneo ya Ukraine ya Sumy upande wa Kaskazini Mashariki, Odesa upande wa Kusini na Kramatorsk Mashariki.
Katika mji wa Kramatorsk, shambulio la bomu lilipiga jengo la makaazi ya watu na kusababisha moto. Hayo ni kulingana na mkuu wa utawala wa kijeshi wa mji huo Oleksandr Honcharenko. Mvulana mwenye umri wa miaka kumi aliuawa katika shambulio hilo huku watu wengine watano wakijeruhiwa.
Mkoa wa Sumy pia haukusazwa katika mashambulizi hayo ya Urusi. Shambulio la droni lilipiga kituo cha mafuta katika mji wa Putyyl na kuwajeruhi watu wanne, akiwemo mvulana wa umri wa miaka mitano. Shambulio lengine la droni lilipiga eneo hilo saa mbili baadaye na kujeruhi watu wengine saba.
Kulingana na mamlaka za mkoa wa Sumy, majengo matano ya makaazi, nyumba mbili za watu binafsi na jengo la biashara liliharibiwa katika mashambulizi hayo.
Kaimu meya Artem Kobzar amethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo na kueleza kwamba yalisababisha uharibifu mkubwa.
Kwa upande mwengine, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema leo kwamba mifumo yake ya ulinzi wa anga ilizuia mashambulizi ya droni 35 yaliolenga miji kadhaa nchini Urusi ikiwemo droni tatu zilizolenga mji mkuu Moscow.