Urusi yaidhinisha mkataba wa uhusiano kati yake na Iran
8 Aprili 2025Bunge la Urusi limepiga kura leo Jumanne kuidhinisha mkataba wa kuimarisha uhusiano wa kisiasa, kijeshi na kiuchumi na Iran, hayo yanajiri wakati ambapo Moscow ikiwa katika harakati za kuimarisha ukaribu wake na mataifa ambayo ni washirika wake wakuu.
Kura ya leo inakuja wakati kukiwa na mvutano mkubwa kati ya Iran na mataifa ya Magharibi na katika kipindi ambacho Urusi pia inapambana kuwa na maelewano na Marekani licha ya vita vyake huko Ukraine.
Soma zaidi:Macron azuru kituo cha misaada kwa watu wa Gaza huko Misri
Akizungumzia kuhusu mkataba huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Andrei Rudenko amesema "Makubaliano haya yanaimarisha uhusiano wa Urusi na Iran hadi kufikia kiwango cha ushirikiano wa kimkakati na wa kina, uhusiano ambao unalenga kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya kipaumbele kwa nchi zote mbili, na kukuza uanzishwaji wa mfumo wa haki wa kimataifa wa pande nyingi."
Mataifa hayo mawili yamekuwa na ushirikiano wa kijeshi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Iran imekuwa ikishutumiwa na Ukraine na nchi za Magharibi kwa kuisambazia silaha Urusi.