Urusi yafanya mashambulizi makubwa zaidi Ukraine
4 Julai 2025Jeshi la anga la Ukraine limesema mashambulizi hayo yalihusisha droni 539 na makombora 11, ambapo takriban watu 23 wamejeruhiwa.
Mwakilishi wa jeshi la anga la Ukraine ameyataja mashambulizi hayo kuwa ni makubwa zaidi tangu Urusi ilipoivamia Ukraine. Milio ya droni na milipuko ilirindima mjini Kyiv, huku raia wakikimbilia kujificha kwenye vituo vya treni.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kwa mara nyingine tena, Urusi inaonyesha kuwa haina nia ya kumaliza vita na vitisho dhidi ya Ukraine na bila shinikizo kubwa la kimataifa, haitabadilisha mwenendo wa uchokozi na uharibifu.
Mashambulizi ya Urusi yameongezeka mwezi Juni, wakati ambapo mazungumzo ya moja kwa moja ya amani kati ya Moscow na Kyiv yamekwama. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andriy Sybiga, alitaja shambulio hilo kama "ishara ya dharau kamili kwa Marekani na wote wanaotaka vita vikome.”
Zelensky atilia shaka msaada wa Marekani
Mapambano kati ya Ukraine na Urusi yanaendelea wakati rais Zelensky akihudhuria tukio la kukabidhi urais wa Baraza la Umoja wa Ulaya kwa Denmark. Katika mkutano huo Zelensky amehimiza Umoja wa Ulaya kuimarisha viwanda vyake vya ulinzi. Huku mashaka kuhusu uendelevu wa msaada wa kijeshi kutoka Marekani yakiendelea.
Zelensky amesema, "Ni wakati wa kuruhusu matumizi ya mabomu yanaoweza kulenga shabaha nyingi kwa wakati mmoja, kutimiza lengo kwa muda mkinachotakiwa ni mipango na uratibu mzuri."
"Kwa sasa wakati ambapo kuna mashaka juu ya Marekani kuendelea kulisaidia bara Ulaya, ni muhimu kuimarisha zaidi ushirikiano wa kufanya kazi pamoja na kuweka muundo utakaohakikisha ufanisi, wa na uwiano kupitia Umoja wa Ulaya, NATO, na hata kwenye mahusiano yetu ya moja kwa moja, kati yetu sisi na pia kati ya bara Ulaya na Marekani.”
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, alisema hatua ya Marekani ya kupunguza msaada ni "ujumbe wa wazi kwa Ulaya kujizatiti zaidi."
Ukraine imekuwa ikijitetea dhidi ya uvamizi wa Urusi kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, huku taifa hilo likidhibitiwa kwa karibu asilimia 20 na majeshi ya Urusi.
Huku haya yakijiri Shirika la ujasusi la Ujerumani BND limetangaza kuwa Urusi imeanza kutumia silaha za kemikali nchini Ukraine, ikiwemo kemikali hatari ya chloropicrin, inayoweza kuwa hatari zaidi katika maeneo yaliyofungwa. BND ilitoa taarifa hiyo kwa ushirikiano na wapelelezi wa Uholanzi.