Urusi yadai shambulio la Sumy lililenga mkusanyiko wa jeshi
15 Aprili 2025Mamlaka za Ukraine zimeripoti kuwa watu 34, wakiwemo watoto wawili, wameuawa katika shambulio la makombora mawili ya balistiki lililotekelezwa na Russia kwenye mji wa Sumy, karibu na mpaka wa Ukraine na Russia.
Zaidi ya watu 100 walijeruhiwa katika tukio hilo lililotokea Jumapili ya Matawi. Hili ni shambulio la pili kubwa katika kipindi cha wiki moja linalowalenga raia.
Russia, kupitia msemaji wake wa Kremlin, Dmitry Peskov, imedai kuwa walilenga mkutano wa maafisa wa jeshi wa Ukraine, na kwamba Kyiv inawatumia raia kama ngao kwa kufanya mikutano ya kijeshi katikati ya miji.
Soma pia: Urusi: Shambulio la Sumy tuliwalenga wanajeshi wa Ukraine
Hata hivyo, Moscow haijatoa ushahidi wowote wa madai hayo, huku viongozi wa Ulaya wakilaani shambulio hilo kuwa ni uhalifu wa kivita.
Wakati hali hiyo ikiendelea, mji wa Kursk ulioko karibu na mpaka wa Ukraine nchini Russia, umetikiswa na milipuko mikubwa siku ya Jumanne.
Kulingana na vituo vya Telegram vya Baza na SHOT, milipuko hiyo imeharibu majengo ya makazi, huku picha zikionesha jengo la orofa likiwa limewaka moto. Chanzo rasmi cha milipuko hiyo bado hakijathibitishwa.