Urusi yadai kuchukua udhibiti wa maeneo mapya Ukraine
14 Agosti 2025Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema vikosi vyake viliteka kijiji cha Iskra na mji mdogo wa Shcherbynivka katika mkoa wa Donetsk, Ukraine — eneo ambalo Kremlin ilidai kulitwaa mnamo Septemba 2022.
Jeshi la Urusi limeongeza kasi ya mashambulizi katika miezi ya hivi karibuni. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mapema wiki hii alikiri kwamba vikosi vya Urusi vimesonga mbele hadi kilomita 10 katika sehemu ya mstari wa mbele karibu na mji wa migodi wa Dobropillia.
Aidha jeshi la Urusi limedai kudungua droni 268 za Ukraine na mabomu manne ndani ya saa 24. Huku Ukraine ikidai kwamba Urusi ilishambulia kwa makombora mawili na droni 45 usiku kucha. Watu wawili walijeruhiwa katika mkoa wa Sumy kaskazini na mmoja katika mkoa wa Kherson, kwa mujibu wa mamlaka za mitaa.