Urusi, Ukraine zaendelea kushambuliana kwa makombora
5 Aprili 2025Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema siku ya Jumamosi (Aprili 5) Ukraine ilikuwa imeishambulia miundombinu ya nishati ya Urusi mara 14 ndani ya masaa 24 yaliyopita, licha ya pendekezo la Marekani linalozuiwa kushambuliwa kwa vinu vya nishati.
Soma zaidi: Shambulizi la Urusi lawauwa watu 18 nchini Ukraine
Shirika la habari la Urusi, TASS, liliinukuu wizara hiyo ikisema kwamba mashambulizi hayo yalisababisha madhara kwenye mikoa ya Bryansk, Belgorod, Smolensk, Lipetsk na Voronezh, na pia kwenye mikoa ya Luhansk na Kherson ambayo ni sehemu ya Ukraine iliyotwaliwa na Urusi.
Watu 18 wauawa Ukraine
Kwa upande wake, Ukraine ilisema kuwa idadi ya waliouawa kutokana na mashambulizi ya Urusi kwenye mji wa Kryvyi Rih imefikia 18, wakiwemo watoto wadogo tisa.
Gavana Serhii Lysak wa mji huo alisema kwamba watu wengine 61 walijeruhiwa kwenye mashambulizi hayo ya siku ya Ijumaa (Aprili 4), akiwemo mtoto wa miezi mitatu.
Soma zaidi: Rutte: Urusi inasalia kuwa tishio kubwa kwa NATO
Kwa mujibu wa gavana huyo, majeruhi 40 bado wako hospitalini, wakiwemo 19 walio kwenye hali mahututi, miongoni mwao ni watoto wadogo wawili.
"Jambo hili haliwezi kusameheka. Linaacha kumbukumbu za kudumu kwa walioathiriwa," alisema mkuu wa baraza la usalama la mji huo, Oleksandr Vilkul
Kryvyi Rih ndio mji aliozaliwa na kukulia Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine, ambaye baada ya mashambulizi hayo aliandika kwenye mtandao wa Telegram: "Kombora lilipiga eneo lililo karibu sana na makaazi ya watu na kuharibu uwanja wa michezo na mitaa ya kawaida."
"Kwa kila kombora, kwa kila shambulizi, Urusi inathibitisha kuwa inachotaka ni vita tu na sio amani." Aliongeza Zelenskyy.
Mamlaka kwenye eneo hilo zilisema mashambulizi hayo yaliliharibu jengo lenye nyumba 20 za watu, zaidi ya magari 30, kituo cha elimu na mkahawa mmoja.
Urusi yadai kuwauwa maafisa wa Ukraine na Magharibi
Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilidai siku ya Ijumaa kwamba ilikuwa imefanya mashambulizi mahsusi kabisa dhidi ya mkahawa mmoja ambako kulikuwa na mkutano kati ya makamanda wa vikosi vya Ukraine na wakufunzi wao kutoka mataifa ya Magharibi.
Soma zaidi: Urusi: Hatujapata mualiko wa mazungumzo ya amani
Kwa mujibu wa jeshi la Urusi, mashambulizi hayo yaliuawa wanajeshi na maafisa wa kigeni 85 na kuharibu magari 20.
Madai hayo hayakuweza kuthibitishwa na vyanzo huru na mkuu wa majeshi wa Ukraine alikataa kuzungumzia tukio hilo.