Urusi: Tunatafari pendekezo la mazungumzo ya amani
21 Julai 2025Msimamo huu wa Urusi umetolewa huku nchi hiyo, saa chache zilizopita kuvurumisha makombora yaliyoilenga Kyiv.
Urusi imeupa uzito mdogo uwezekano wa kurejea kwenye meza ya mazungumzo na Ukraine na kusema kuwa pande zote mbili zina mitazamo mikali tofauti.
Juhudi za kufikia suluhu ya kidiplomasia ya mzozo huo wa miaka mitatu zinasuasua baada ya raisi Donald Trump wa Marekani kuzishinikiza pande zote mbili kufanya vikao vya ana kwa ana aliporejea madarakani mwanzoni mwa mwaka huu.
Wawakilishi wa pande hizo mbili walikutana mara ya mwisho zaidi ya mwezi mmoja uliopita mjini Istanbul na kubadilishana mawazo kuhusu rasimu ya vipengee vya mkataba huo wa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari,msemaji wa ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov,alifafanua kuwa sasa wanahitaji kubadilishana mawazo kuhusu rasimu hizo mbili ambazo zinatofautiana kwa kiasi kikubwa na kwamba kibarua kikubwa kiko mbele.
Kufikia sasa, matunda ya mazungumzo hayo ni kubadilishana wafungwa ila kasi ya kusitisha vita imeisha nguvu.Rais Trump aliyeelezea kuchoshwa akili na Urusi, alitowa muda wa siku 50 kwa Vladimir Putin kufikia mwafaka au kuwekewa vikwazo vikali vya kiuchumi.
Wiki iliyopita, Rais Zelensky alitoa wito kwa mazungumzo hayo kufanyika wiki hii.
EU yaweka mbinyo wa vikwazo zaidi kwa Urusi
Umoja wa Ulaya uliafikiana ijumaa iliyopita kuiwekea Urusi vikwazo vipya vinavyodhamiria kuziandama benki zake na kuiongeza gharama ya vita ili kuishinikiza Moscow.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Jean-Noel Barrot aliyewasili Kyiv wakati bado mji unafuka moshi alisema vikwazo ambavyo vimeaidhinishwa ni vikali zaidi kwa Moscow.
''Bei ya juu ya mafuta na vikwazo dhidi ya bidhaa za mafuta yaliyosafishwa kutokea mataifa ya tatu yanayosafisha mafuta ya Urusi,pato la Urusi la mafuta na huduma za fedha vitamlazimu Putin kubadili mkondo wake.''
Hivi sasa wakati Urusi ikidai kuwa tayari kushiriki duru mpya ya mazungumzo,Duru zinaeleza kuwa watu wawili waliuawa hii leo Jumatatu kwenye wimbi jipya la mashambulizi yaliyofanywa na nchi hiyo ambayo Ukraine imeyaelezea kuwa hujma dhidi ya ubinadamu.
Wilaya sita za Kyiv zilishambuliwa kwenye mashambulio hayo mapya. Meya wa Kyiv Vitali Klitschko alifahamisha kuwa mfumo wa kupambana na makombora unafanyakazi na kwamba wakaazi wasalie majumbani mwao.
Ukraine inataka vita kusitishwa mara moja na Urusi kuheshimu azma yake ya kutaka kujiunga na NATO na Umoja wa Ulaya.