Urusi: Shambulio lililenga wanajeshi wa Ukraine
14 Aprili 2025Mashambalizi hayo ya Urusi yalifanyika kilomita 30 ndani ya mpaka wa Ukraine na Urusi. Miongoni mwa watu waliouawa kutokana na makombora ya Urusi walikuwa watoto wawili huku idadi ya waliojeruhiwa ikifikia watu 119.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa Ukraine wakiyataja kuwa ya pili hatari katika kipindi cha wiki moja tu. Alipohojiwa kuhusu taarifa za mashambulizi hayo, msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amedai kuwa majeshi ya Urusi yalilenga kushambulia vituo vya kijeshi tu:
"Mnajua kwamba sisi hatutoi taarifa za operesheni za kijeshi katika utawala. Ninachoweza kukariri na amabacho rais wetu na wawakilishi wa majeshi wamefahamisha katika taarifa ni kwamba mashambulizi yetu hulenga vituo vya wanajeshi na maeneo jirani yake."
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa waliushambulia mkusanyiko wa maafisa wa ngazi za juu wa Ukraine. Imekosoa utawala wa Kyiv kuwatumia raia kama kinga wakati wa kuendesha mkutano wa kijeshi katikati kwa mji huo wa Sumy. Wizara hiyo imetaja kuwaua wanajeshi zaidi ya 60 lakini haikutoa ushahidi kuthibitisha madai yake hayo.
Katika ujumbe wake kwenye majukwaa ya kijamii, Rais wa Urkraine Volodymyr Zelensky ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua kufuatia mashambulio hayo akielezea kuwa la kwanza liliharibu majengo ya chuo kikuu na lingine likaripukia kwenye barabara kuu.
Soma pia:Rais Zelensky amuomba Trump aitembelee Ukraine
Amesema kuwa shinikizo dhidi ya Urusi ndilo litamfanya Rais Vladimir Putin kuacha mashambulizi hayo na kutaka vikwazo viwekwe dhidi ya sekta zinazofadhili upatikanaji wa zana za mauaji za Urusi.
Waziri wa masuala ya kigeni wa Poland, Radek Sikorski, ambaye nchi yake inashikilia kiti cha urais wa Umoja wa Ulaya, ameyataja mashambulizi ya Urusi kuwa dharau na kejeli kwa mwitikio wa utawala wa Kyiv kukomesha vita kama ilivyopendekezwa na Marekani zaidi ya mwezi mmoja uliopita.
Waziri wa masuala ya kigeni wa Finland, Elina Valtonen, naye ametoa mtazamo kama huo akielezea kuwa mashambulizi kwenye mji wa Sumy yamefanyika siku chache baada ya mjumbe wa Rais Donald Trump, Steve Witkoff, kufanya mazungumzo mjini St. Petersburg na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Ametaja mashambulizi hayo kudhihirisha kuwa Urusi haina haithamini mchakato wa amani na pia haijali maisha ya binadamu. Huku Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Ufaransa Jean-Noël Barrot akisema kuwa Rais Putin hana kusudio lolote kukubali usitishaji vita, amehimiza Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kali za vikwazo dhidi ya Urusi ili kuathiri uchumi wake.
Hadi sasa Umoja wa Ulaya umeiwekea Urusi vikwazo 16 na wanajadili cha 17. Ila kikwazo hicho kinacheleweshwa kwa kuwa kinaathiri pia uchumi wa mataifa kadhaa ya bara hilo.
Ujerumani yatoa mwito wa Ukraine kupewa silaha zaidi
Akiyataja mashumbulizi hayo kuwa uhalifu wa hali ya juu wa kivita, Kansela mteule wa Ujerumani, Friedrich Merz, kwa mara nyengine amekariri mwito wa kupeleka makombora ya masafa marefu ya Taurus nchini Ukraine. Kansela anayeondoka Olaf Scholz alikata kufanya hivyo.
Alipoulizwa kutoa tamko kuhusu wazo la Merz, msemaji wa Kremlin amesema kuwa hatua hiyo itazidisha hali ya kivita dhidi ya Ukraine.
Badala yake amewakosoa viongozi wa Ulaya kjwa kushindwa kutafuta njia za kuanzisha mazungumzo ya amani na kuendeleza vita hivyo.
Soma pia:Viongozi wa dunia walaani shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine
Mwezi huu pekee majeshi ya Urusi yamefanya mashambalizi ya mabomu 2,800 kwenye ardhi ya Ukraine, yakarusha droni 1,400 na takribani makombora 60 sehemu mbalimbali za nchi hiyo.
Shambulio dhdi ya Sumy linafuatia lile la tarehe 4 Aprili zililosababiusha vifo vya watu 20 wakiwemo watoto 9 katika mji wa Kryvyi Rih anakotokea Rais Zelensky.