Urusi na Ukraine zashambuliana licha ya juhudi za upatanishi
6 Mei 2025Urusi iliishambulia mikoa miwili ya mashariki mwa Ukraine ikiwemo Sumy na kuwaua watu watatu. Hayo yalitangazwa na utawala mjini Kyiv.
Urusi nayo kupitia viongozi wake imesema mashambulizi ya Ukraine yamewaua watu watatu katika mkoa wake wa mpakani wa Kursk.
Inaarifiwa vikosi vya Ukraine vilifyetua makombora kuulenga mkoa huo na kisha wanajeshi wake kuingia kwenye ardhi hiyo ya Urusi kwa kutumia magari ya kivita katika eneo lililotegwa mabomu.
Maafisa wa Ukraine hawajazungumzia chochote juu ya madai ya vikosi vyake kuushambulia mkoa huo wa Kursk. Taarifa hizo lakini yumkini zitawastua wengi ndani ya Urusi.
Ukraine ilifanikiwa mwaka jana kukamata sehemu kubwa ya ardhi ya Urusi kwenye mkoa huo wa Kursk lakini Moscow ilitangaza mwezi Aprili kuwa imeikomboa ardhi hiyo.
Ukraine yailenga Moscow kwa usiku wa pili mfululizo
Katika hatua nyingine Ukraine ilifanya shambulizi la droni usiku wa kuamkia leo likiulenga mji mkuu wa Urusi, Moscow.
Hilo ni shambulizi la usiku wa pili mfululizo baada ya hapo jana Urusi kusema ilidungua droni nne zilizokuwa zinaelekea Moscow.
Meya wa mji huo mkuu Sergei Sobyanin amesema shambulizi la usiku wa kuamkia lepo lilhusisha droni 19 ambazo zote zilidunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga.
Afisa huyo amesema hakuna vifo wala uharibifu uliotokea lakini shambulizi hilo lililazimisha kufungwa kwa muda kwa viwanja vikubwa vitatu vya Moscow.
Ukraine haijasema chochote kuhusu hujuma hizo lakini mara kadhaa viongozi wa nchi hiyo wamesema wananuwia kuiharibu miundombinu yote muhimu inayoiwezesha Urusi kuendelea kuishambulia ardhi ya Ukraine.
Juhudi za kutafuta usitishaji mapigano zagonga mwamba
Kumekuwa na juhudi za kidiplomasia za kujaribu kusimamisha mapigano kati ya pande hizo mbili zinazoongozwa na Marekani. Rais Donald Trump alipendekeza hivi karibuni usitishaji mapigano wa bila masharti kwa siku 30 mpango ambao Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliuridhia.
Hata hivyo Rais Vladimir Putin wa Urusi aliukataa na badala yake akatangaza usitishaji mapigano wa upande mmoja kwa muda wa siku tatu kuanzia Alhamisi usiku hadi mchana wa Jumapili inayokuja.
Usitishaji huo unarandana na Gwaride la Ushindi la kila mwaka kuadhimisha kumalizika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Siku hiyo husherehekewa nchini Urusi kila ifakapo Mei 6. Rais Zelensky wa Ukraine amekataa usitishaji huo mapigano uliotangazwa na Putin.
Amesema ni kitendo cha "hadaa isiyo mfano kwamba Urusi imechagua kusitisha mapigano ili kupisha sherehe za Mei 9 lakini bado vikosi vyake vinaendelea kuishambulia Ukraine."