Urusi na Ukraine zashambuliana kwa makombora usiku kucha
1 Mei 2025Urusi leo imeripoti vifo vya watu saba na wengine 20 wamejeruhiwa baada ya droni za Ukraine kushambulia eneo la soko lenye shughuli nyingi huko Oleshky, sehemu ya mji Kherson wa Ukraine inayodhibitiwa na Urusi.
Katika hatua nyingine Ukraine nayo imesema kwamba Urusi imefanya shambulizi katika mji wa bandari wa Odesa nchini Ukraine na kuwaua watu wawili na kujeruhi wengine zaidi ya 15. Mashambulizi hayo pia yalizusha moto ulioharibu miundombinu.
Soma zaidi:Ukraine na Marekani zasaini"makubaliano ya uwekezaji"
Taarifa ya jeshi la anga la Ukraine imesema Urusi ilirusha makombora matano na droni 170 wakati wa mashambulizi yake ya usiku wa kuamkia leo yakilenga maeneo mbalimbali ya Ukraine.
Mashambulizi hayo yametokea saa chache baada ya Ukraine na Marekani kutia saini "makubaliano ya uwekezaji" yatakayoiruhusu Marekani kuchimba madini ya Ukraine.