Urusi na Ukraine zakubaliana kusitisha mashambulizi Baharini
26 Machi 2025Marekani imefikia makubaliano tofauti na Ukraine na Urusi, ambapo nchi hizo zimekubali kusitisha mashambulizi baharini na dhidi ya miundombinu ya nishati.
Rais Donald Trump ameahidi pia kushinikiza kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo dhidi ya Moscow, hususan katika sekta ya kilimo na mbolea, suala ambalo limekuwa likidaiwa na Urusi kwa muda mrefu.
Hata hivyo, Urusi imesema makubaliano hayo kuhusu Bahari Nyeusi hayatatekelezwa hadi baadhi ya benki zake zirejeshwe katika mfumo wa kifedha wa kimataifa.
Soma pia: Vladmir Putin atowa masharti ya usitishaji vita
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, amesisitiza kuwa makubaliano hayo hayatakiwi kutegemea kuondolewa kwa vikwazo, akiiita kauli ya Kremlin jaribio la kujaribu "kuchezea" utekelezaji wa makubaliano hayo.
Mazungumzo haya, yaliyofanyika Saudi Arabia baada ya Trump kuwasiliana na marais wote wawili, yanaonekana kama hatua ya kwanza muhimu kuelekea lengo lake la kusimamisha vita nchini Ukraine, vilivyoanza miaka mitatu iliyopita.